
TOWNSHIP Rollers imekiri kuwa kwa kiwango walichoonyesha Simba jana Jumamosi mjini hapa kwenye mechi ya kirafiki iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, ni dhahiri kwamba mabingwa hao wa Tanzania wameiva.
Katika mchezo huo uliochezwa asubuhi, Simba ilionyesha ubora kwenye fiziki, kukaba kwa umakini kuanzia mbele pamoja na soka la kufunguka muda mwingi wa mchezo huku Sydney Magagane ambaye ni meneja mkuu wa Rollers akitikisa kichwa na kuwaambia vigogo wa Simba kwamba vijana wako vizuri.
Mbali na hilo, Kocha wa Wabotswana hao, Tomas Trucha ambae ni raia wa Czech alimfuata Mbelgiji wa Simba,Patrick Aussems na kuteta nae mara kadhaa na kusifia ubora wa kikosi cha mnyama haswa kwenye fiziki na kukaba.

Aussems aliwaachia wachezaji wake wacheze soka la kufunguka kwa umahiri mkubwa, kushambulia na pasi za haraka ambazo ziliwatoa jasho Rollers wanaojiandaa kucheza na Yanga kwenye mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Agosti 10 Jijini Dar es Salaam.
Kiwango cha Simba kilimkosha Trucha ambaye alikiri kwamba mchezo huo ulikuwa na manufaa makubwa kwake na ni miongoni mwa mechi ambazo zitamjenga sana kabla ya kuikabili Yanga.
Trucha alikaa dakika kadhaa kabla na baada ya mchezo huo kuzungumza faragha na Aussems ambapo licha ya kumsifia kutokana na ubora wa kikosi chake lakini alikuwa akimdodosa kuhusu Yanga ingawa alichomwambia kitaalamu ilibaki siri yao kwani wote walificha.
“Simba walikuwa wanakaba hadi golini kwetu, walikuwa kwenye nusu yetu muda mwingi, huku wakikimbia na
kupambana kushinda mchezo, kiasi cha kufikia kumchosha hadi mwamuzi,” alisema Trucha.
“Lakini cha muhimu tumepata matokeo mazuri na kuepuka majeraha,” aliongeza kocha huyo ambaye bado timu yake itazidi kupasha Sauzi kwa wiki mbili zijazo. Trucha na vigogo wengine waliokuwa kwenye uwanja huo walikuwa wakido dosa ishu za Yanga ya Mwinyi Zahera na mastaa wapya waliosajiliwa msimu huu akiwemo, Patrick Sibomana ambaye huko Moro anatupia hat-trick tu.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Royal Bafokeng mjini hapa, Simba ilitawala muda mwingi wa mchezo huku wachezaji wake wakionekana kuwazidi lishe wapinzani wao.
Simba katika dakika 45 za mwanzo ilionekana kuwa na utulivu mkubwa na kushambulia kwa kasi kwa kutumia pasi mpenyezo ambazo ziliashiria kwamba kambi ya hapa imekuwa na manufaa.
Kipindi cha kwanza Township ilitumia akili za ziada kusaka mipira huku wachezaji wao wakionekana wenye kasi, pumzi na wasiochoka ingawa miili midogo ilikuwa ikiwaponza kuwatuliza watu walioshiba kama Meddie Kagere.
Dakika ya 33, Beno Kakolanya ambaye ndiye mechi yake ya kwanza nzito ndani ya Simba alipangua penalti ya Kitso Mpuisang baada ya mabeki wa Simba kuunawa mpira kwenye harakati za kuokoa.
Mpuisang na Maano Ditshupo walikosa nafasi kadhaa za magoli ya wazi kutokana na mchecheto walipokuwa wakikaribia kwenye boksi la Simba na kujikuta wakipaisha au kupiga mashuti dhaifu ambayo Beno aliyapangua kiufundi.
Huku akionekana kuwatoa jasho mabeki wa Township muda wote, dakika ya 58 Francis Kahata alipandisha shambulizi moja la nguvu lenye uhalali wa thamani yake na ndipo mkali Meddie Kagere akatupia bao la kuongoza. Rollers walitulia na kucheza kwa kujilinda huku wakitumia zaidi winga zao kupandisha mashambulizi ambayo dakika ya 70, Serameng akawafutia aibu ya kipigo, ingawa Simba walionekana kuanza kuzidisha mpira wa burudani na kocha akifanya mabadiliko ya hapa na pale kumsoma kila mchezaji.
