
Leo Jumatano, Azam FC inaikaribisha Yanga SC uwanja wa Chamanzi katika msako wa pointi tatu ambazo kila timu inahitaji kusepa nazo, Azam FC ilitoka kushinda 2-1 dhidi ya Namungo FC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Ilulu, huku Yanga ikiifunga KMC 2-0.
Moto upo kwenye safu ya ushambuliaji ambapo rekodi zinaonesha yule aliyekuwa wa mwisho kuifunga Yanga na ikapoteza pointi mazima kwenye ligi amerejea kwenye ubora ambaye ni Prince Dube alifanya hivyo, ilikuwa ni Aprili 25, 2021 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, ubao ulisoma Yanga 0-1 Azam FC, msimu huu, Dube alifunga bao lake la kwanza kwenye ligi Uwanja wa Namungo, hivyo moto wake unaweza kuendelea leo ama maji yakapoa.
Mchezaji wa kuchungwa zaidi kwenye kikosi cha Yanga ni Fiston Mayele ambaye ana kasi kubwa na jicho la kufunga akiwa ni namba moja kwa utupiaji ndani ya kikosi cha Yanga, ametupia mabao 10 na pasi tatu za mabao, amehusika katika mabao 13 kati ya 31 ambayo yamefungwa na Yanga iliyo nafasi ya kwanza na pointi 48, amecheza mechi 18.
Timu zote mbili zinahitaji kuwaacha mashabiki kwa mtindo wao ambapo Azam FC inahitaji kuwapa tulizo baada ya ule mchezo wa kwanza kunyooshwa mabao 2-0 Uwanja wa Mkapa kwa upande wa Yanga, wao wanahitaji kuendelea pale ambapo waliishia ili wasitibue rekodi yao wakati huohuo ikiwa Azam FC itashinda mchezo huu, itakuwa ni timu ya kwanza kuifunga Yanga ndani ya ligi msimu huu baada ya kucheza mechi 18 bila kufungwa.

Yanga hesabu zao ni kushinda ili kufungua njia ya kufikia ulipo ubingwa ambao unashikiliwa na Simba iliyo nafasi ya pili, kwa sasa Yanga inaonekana kuwa bora kila idara kwa msimu huu tofauti na Azam FC, ukianza na ile safu ya ushamuliaji, ambayo imetupia mabao 31 huku Azam FC ikitupia mabao 22, tofauti mabao 9.
Abdi Hamid Moallin, Kocha Mkuu wa Azam FC, anasema: “Yanga ndiyo timu bora nchini kwa sasa, unapaswa kucheza na walio bora ili kuwa bora. Mchezo wetu dhidi ya Yanga tunataka kuuchukulia tofauti kama ule wa Namungo.
“Alama 20 mbele yetu na bado hawajapoteza, hilo ni kubwa, hivyo kwetu ni fursa kucheza nao na tunajiandaa kwa ajili ya mchezo huo.”
Nasreddine Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga, aliliambia Spoti Xtra kwamba: “Ninatambua kwamba kuna mechi ngumu zinakuja kwani baada ya KMC inafuata Azam FC, huu ni mchezo ambao unahitaji umakini mkubwa na kikubwa ni ushindi.
“Haitakuwa kazi rahisi kwetu, nimewaambia wachezaji kuwa kazi ni moja, kutafuta ushindi na inawezekana kwa kuwa mimi ninapenda kuona tukicheza na kushinda kwa vitendo.”
Yanga iliifunga Azam FC mabao 2-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza na inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa na alama 48 Azam FC yenyewe imekusanya alama 28 katika Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa nafasi ya tatu.