
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar, leo Agosti 15, 2019, imeamuru maombi ya zuio la muda la kuapishwa kwa mbunge mteule wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM) na maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kusikilizwa Agosti 23, 2019.
Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe taarifa yake ya kumvua ubunge.
Upande wa utetezi uneiomba Mahakama Kuu ya Tanzania chini ya hati ya dharura itoe amri ya kusitisha mchakato wa kuapishwa kwa mbunge huyo mteule wa Singida Mashariki,. Maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019 yametajwa leo Agosti 15, 2019, mbele ya Jaji Sirilius Matyupa ambapo anawakilishwa na jopo la Mawakili wanne akiwemo Peter Kibatala, huku upande wa wajibu maombi ukiwakilishwa na mawakili wanne akiwemo Wakili wa Serikali Mkuu, Vincent Tango.
Katika maombi hayo, Wakili wa utetezi ambaye ni peter Kibatala ameomba mwongozo wa mahakama ili waweze kuzungumzia ombi la kusitisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, lakini ombi hilo likapingwa na mawakili wa Serikali wakidai kuwa kwa sasa sio muda muafaka wa kuanza kulisikiliza.
Pia upande wa jamhuri wameomba muda wa siku nane waweze kuwasilisha hati ya kiapo kinzani pamoja na hati ya maelezo kinzani kabla ya maombi hayo kupangiwa siku ya kuanza kusikilizwa.
Wakili Tango amesema kuwa kwa kuwa shauri hilo linahusisha mhimili mwingine, ambao ni Bunge basi wanahitaji kupata muda wa kushauriana na Bunge (Spika) ili kuweza kuandaa kiapo kinzani.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, ingawa amesema kuwa hana tatizo na wajibu maombi kuomba muda wa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani, amesema kuwa muda wa siku nane walioomba ni mrefu kulingana na mazingira ya kesi hiyo, ambayo inabidi isikilizwe na kutolewa uamuzi ndani ya siku 14.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Sirilius Matyupa amesema atatoa uamuzi wa kusitisha mchakato wa kuapishwa kwa mbunge huyo mteule baada ya kusikiliza maombi yote Agosti 23, 2019.
Siku ya Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, akisema kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.
