×

JPM Akabidhiwa Uenyekiti SADC, Ahutubia – Video

MKUTANO wa siku mbili wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeendelea jijini Dar es Salaam ambapo Rais John  Magufuli amekabidhiwa uenyeketi wa jumuiya hiyo na Rais Hage Geingob wa Namibia aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo.

 

Kabla ya kukabidhi uenyekiti,  Geingob amesema Tanzania ni nchi yenye amani na uchumi wake unaendelea kukua kwa kasi kubwa kutokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ya kimkakati  na uwekezaji katika viwanda kwa sasa ambao unachangia kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana.

 

Nsaye akifungua mkutano huo ambao umehudhuriwa na marais 11 wa SADC, Magufuli amesema ni fursa nzuri kwa Watanzania kuendelea kulitangaza taifa kupitia mkutano huu wa kihistoria.

 

 

Amesisitiza kwamba mafanikio ya maendeleo ya viwanda ni dira nzuri na mfano wa kuigwa kwa nchi wanachama wa SADC hivyo ni fursa nyingine muhimu kwa nchi wanachama kujifunza kwa Tanzania ambayo itakuwa mwenyekiti.

 

Pia ametangaza lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya nne itakayotumika katika vikao mbalimbali vya jumuiya hiyo.

 

“Najua hii si kazi ndogo na inakuja na matarajio makubwa sana, lakini niwaahidi nitajitahidi sana kufikia matarajio yenu, na kwa manufaa ya jumuiya yetu. Niwaahidi wenzangu ile Tanzania ambayo mlikuwa mnaijua kwa watangulizi wangu, niwaahidi itaendelea kuwa hiyohiyo, tangu ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Mzee Kikwete.

“Moja ya jumuiya ambazo zina amani kubwa sana, ni hii jumuiya yetu ya SADC, japo nikiri kuwa kuna baadhi ya nchi zetu za SADC bado zinakabiliwa na migogoro ya mara kwa mara. Kama mwenyekiti wa SADC nitahakikisha ninashirikiana na wanachama wote, kuhakikisha amani inaendelea kuwepo.

 

“Hivi karibuni nilitembelea nchi nne za SADC nikakutana na nchi ambazo zina ukame kwa hiyo kulikuwa na njaa, nilichoshangaa ni ndugu zetu kuweka nia ya kuagiza chakula nje ya Afrika, wakati Tanzania hapa tuna chakula cha kutosha. Moja ya matatizo makubwa ambayo mimi naona ni kuyapigania  ni kupanua sekta ya viwanda kwenye jumuiya yetu.

“Kabla sijamaliza naomba niseme jambo moja, ambalo nimekuwa nikiwaambia wenzangu kwamba nchi yetu si masikini; tuna utajiri mkubwa sana, tuna rasilimali nyingi sana. Kwa mawazo yangu binafsi, nadhani kama tukifanya kazi kwa pamoja kama jumuiya ya SADC, nadhani uchumi utakua zaidi ya asilimia 3.1.

 

“Inapofikia hatua tukiona tunapelekea malighafi nje ya nchi, kwa kuwa zinauzwa kwa gharama ndogo lazima tujue pia tunachokifanya ni kupeleka ajira za watu wetu nje ya nchi. Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja mimi nikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya hii ya SADC, nitahakikisha masuala ya viwanda yanapewa kipaumbele.

“Zimbabwe wamekuwa kwenye vikwazo kwa muda mrefu, hiki kifungo tunaathirika sisi wote,  kupendekeza kupitia mkutano huu kuiomba jumuiya za kimataifa iiondolee vikwazo Zimbabwe, na nawaomba wanachama wote tulisemee hili. Napendekeza vikwazo vilivyowekwa na jumuiya za kimataifa dhidi ya Zimbabwe viondolewe, na jumuiya hii ya SADC kupaza sauti juu ya suala hili, hawa ni ndugu zetu na kwa sasa wanafanya vizuri.”

 

Mbali na marais 11 wa SADC mkutano huo utakaofanyika leo na kesho, umehudhuriwa na marais na mawaziri wote wastaafu  na viongozi wengine waandamizi wa vyama mbalimbali vya siasa.

 

FUATILIA MKUTANO HUO HAPA