JESHI la Polisi mkoani Iringa, limesema kuwa limebaini tukio lililotokea la ‘mchawi’ kudondoka juu ya paa la nyumba ya mchungaji eneo la Ilula ni la kutengenezwa ambapo mwanamke aliyefanya hivyo alilipwa pesa ili kutengeneza sakata hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Juma Bwire, amesema kuwa mama huyo ambaye alijitambulisha kwa jina la Kabula Masunga hapo awali alidanganya kwamba jina lake kamili ni Magreth Simon ili kukwepa ukweli.
Amesema awali Magreth Simon alisema kuwa anatokea Morogoro lakini ni mkazi wa Sengerema kkoani Mwanza kama ambavyo imebainisha mumewe, Jeremia Yustas, baada ya kutoa taarifa makao makuu ya Polisi mkoani Iringa.
Aidha, Yustas amesema BKabula aliaga kuwa anaelekea Musoma kwa ajili ya kujengea makaburi ya ndugu zake na kwamba alishangaa kuona ameshikwa mkoani Iringa kwa uchawi.
Nao wakazi wa mji mdogo wa Ilula wamesema kitendo hicho hakivumiliki, hna kwamba wananchi wanatakiwa kuwa makini kwa kuwa mama huyo angeweza kuuawa na wananchi ambao wanaamini ushirikina.
Mapema mwezi Agosti, jeshi la polisi mkoani Iringa lilimkamata mama huyo ajulikanaye kwa jina la Kabula Masunga akiwa amelala juu ya paa la nyumba ya Mchungaji Jeremiah Charles katika halmashauri ya mji mdogo wa Ilula, wilayani Kilolo, mkoani Iringa baada ya wananchi kumtuhumu kuwa mchawi.