
DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, DC Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ ameandika historia baada ya kumkabidhi nyumba mama aliyejifungua watoto mapacha walioungana, Ester Simon (24), mkazi wa Kijiji cha Mzenga mkoani humo aliyekuwa akiishi kwenye nyumba chakavu. Akizungumza na Gazeti la Ijumaa, Jokate alisema, hakuna kitu kizuri kama kuwasaidia wengine ambao wapo kwenye matatizo makubwa zaidi kuliko yako, kitendo cha kumpa mama huyo nyumba ya kuishi yeye na wanaye ambao huko
nyuma walikuwa wameungana kimemfanya ajione mwepesi. Jokate alisema kuwa, amejikuta akipata usingizi mzuri baada ya kutimiza ahadi hiyo ya kumsaidia mama huyo na wanaye kwa kupitia wafadhili mbalimbali aliowatafuta yeye.
“Kitu kizuri sana kwenye dunia hii ni kusaidia wengine, lakini mimi kama kiongozi ni lazima nihakikishe mwananchi wangu anaondokana na shida kubwa ambayo ingeweza kupoteza hata uhai wa watoto wake ambao nao walizaliwa wakiwa na matatizo hivyo kukamilisha nyumba ni jambo kubwa lililokosha moyo wangu,” alisema Jokate.
Alisema kuwa, nyumba hiyo yenye vyumba viwili vya kulala, varanda, jiko na sebule pia ina maji na umeme, kwa mama huyo na wanaye mapacha ni kitu kikubwa hivyo anawashukuru alioshirikiana nao bega kwa bega kama African Reflections Foundation ambao ndiyo wamemjengea nyumba hiyo.
Katika hilo pia tayari mkuu wa mkoa huo (Mhandisi Evarist Ndikilo) ameshawatafutia bima ya afya watoto hao kwa miaka 10 na kuwafungulia akaunti katika Benki ya BOA (Bank of Africa) ambapo benki hiyo tayari imewawekea kiasi cha shilingi milioni mbili huku Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa imekubali kuwahudumia watoto hao bure kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa wana changamoto yoyote.
Stori: IMELDA MTEMA,Ijumaa