
KWA neema ya Mungu nimefika hapa nilipo maishani mwangu, ndicho ninachoweza kusema, lakini pamoja na neema hiyo, sheria ilikuwa ni hii; NEEMA YA MUNGU + KANUNI = MAFANIKIO!
Nimefundisha mara nyingi kwenye mikutano yangu ya kwamba mambo haya mawili ni lazima yaende pamoja, KANUNI peke yake zikitumika bila NEEMA YA MUNGU hakuna kinachoweza kutokea maishani mwako, huu ndiyo ukweli.
Ni kweli kwa NEEMA tunabarikiwa mno, lakini bila kutumia KANUNI fulani udhihirisho wa Baraka za Mungu maishani mwetu hauwezi kuonekana. Hapa nina maana kwamba ni lazima mambo fulani yafanyike pamoja na NEEMA hiyo ndipo upate kubarikiwa.
Mfano mzuri wa kudhihirisha sheria hii ni kama baba yako alifariki dunia ukiwa mtoto mdogo na kukuachia utajiri wa bilioni mia mbili kwenye akaunti, fedha hizo ingawa ni zako bado ni lazima upitie mchakato fulani ndiyo uzipate, mfano, lazima uende benki kufuata taratibu za kisheria ili uweze kumilikishwa kisheria ingawa kweli ni zako. Usipofanya hivyo, fedha hizi zitabaki kwenye akaunti bila wewe kufaidika nazo.
Hivyo ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa mafanikio, lazima pamoja na NEEMA YA MUNGU, KANUNI kadha wa kadha zitumike ili uweze kuzipata BARAKA ZA MUNGU. Wakristo wengi sana wameishi maisha duni ingawa walitakiwa kuishi maisha ya kitajiri kwa sababu tu hawaelewi jinsi ya kutumia sheria hii ya NEEMA YA MUNGU + KANUNI = MAFANIKIO!
Ukisoma katika Biblia kwenye Kitabu cha Muhubiri 10:7; Neno la Mungu linasema wazi kuwa; “Nimeona watumwa wamepanda farasi na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.”
Watu waliotakiwa kuishi kama wafalme, wanaishi kama watumwa na waliotakiwa kuishi kama watumwa wanaishi kama wafalme, kwa nini? Hapa hakuna jibu lingine zaidi ya kwamba waliotakiwa kuishi kama watumwa wanaishi kama wafalme kwa sababu wanazijua kanuni na wanazitumia maishani mwao.
Huu ni ukweli, yeyote anayeijua kanuni na anaitumia, bila kujali ameokoka au hajaokoka, lazima aishi kama mfalme! Na asiyeijua kanuni au anaijua, lakini haitumii ingawa alitakiwa kuishi kama mfalme ataishi maisha yake kama mtumwa, hivyo basi ndugu zangu, ni lazima tujifunze kanuni za mafanikio. Nilipoamua kutafuta mafanikio nililazimika kuzifahamu kanuni hizi na kuzitumia maishani mwangu, ukizifahamu na ukazitumia, bila kujali umeokoka au hujaokoka, una digrii au huna digrii; utaishi kama mfalme!
Ndiyo maana maishani unawashuhudia watu wenye elimu kubwa kabisa, wengine wana digrii au PHD za uchumi, lakini bado wanaishi maisha kama watumwa, huku watu ambao pengine hawakuingia hata darasani, lakini walizifahamu tu kanuni barabarani, wakazitumia, ndiyo wanawaajiri wenye PHD.
Moja ya kanuni ambayo mimi ndugu yenu ninaifahamu na nimeitumia sana maishani mwangu ni KANUNI ya kusaidia maisha ya watu wengine kubadilika, yaani kila siku kujiuliza; “Hivi nawezaje kutumiwa na jamii yangu?” Au “Ninawezaje kuleta tofauti katika maisha ya watu wengine?” Mtu ambaye hujiuliza maswali haya na kupata namna ya kusaidia wengine, hakika hawezi kukwama maishani mwake maana kama vile ambavyo yeye huwasaidia wengine, Mungu atamwamini na vitu ili aweze kumwakilisha vizuri hapa duniani.
Hivi huwa hushangai kwamba watu bahili na wachoyo sana huwa hawasongi mbele kifedha? Wapo watu hapa duniani hawatumii vitu vyao kabisa na watu wengine, lakini hawapigi hatua maishani, tofauti na watu ambao kila siku wanawaza jinsi ya kusaidia watu wengine kunyanyuka, ambao kila siku utawasikia wanazidi kusonga mbele, hii ni siri kubwa sana ya mafanikio ilimradi tu uwe unamfanyia Mungu siyo kufanya ili wanadamu waone.
Nawaelezeni yote haya kwa lengo moja tu; kuwafanya mzijue siri za mafanikio, ziko kama kumi hivi, ukitafuta kitabu changu cha Sheria Kumi Zilizothibitishwa za Kutoka Kwenye Umasikini Kwenda Kwenye Utajiri, utazisoma zote na kuzielewa na kama utazitumia, nakuhakikishia kwamba haijalishi hapo ulipo leo, haijalishi kiwango chako cha elimu, haijalishi kabila wala rangi yako ya ngozi; UTAFANIKIWA UTAKE USITAKE!
Baada ya kuwa na NEEMA YA MUNGU sasa ni jukumu lako kutafuta KANUNI zitakazokupeleka kwenye mafanikio;
Mafanikio ya kweli yanaanza na wewe. Hivyo, kujiamini ni msingi mzuri utakaokufanya utambue uwezo wako katika kufanya jambo fulani. Amini uwezo wa kufanya jambo hilo uko mikononi mwako. Usijishushe, jipime kwa mengi mazuri unayoweza kufanya, ikatae roho ya kujiona huwezi.
Kujiamini ni msingi wa pili mkuu wa mafanikio. Uoga wa kuthubutu ni kikwazo kikuu kinachowarudisha wengi nyuma na kujikuta hata kuanza safari ya mafanikio hawawezi. Jambo lolote zuri na kubwa huwa gumu kufanya na ni rahisi kuhisi haliwezekani. Usikubali kushindwa bila kujaribu. Thubutu kwa dhati na weka nguvu yako na akili yako yote katika uthubutu huo. Hata hivyo, katika uthubutu huu, unapaswa kupima vizuri ili uchukue ‘calculated risk’ na siyo ‘just risk’.
Kumbuka, ukishindwa kupanga ujue umepanga kushindwa. Kuwa na mipango inayopimika na kutekelezeka kwa kiwango cha juu. Usiwe na mipango tu mikubwa ambayo hata utekelezaji wake hauwezekani.
Unapopanga fikiria wapi utapata rasilimali na jinsi ya kutelezeka, lakini pia mpango wako ukupe uwezo wa kuutathmini na kujipima mwisho wa kazi hiyo. Hata hivyo, mipango haitakuwa na maana kama hautaitekeleza kwa ufanisi. Ukishindwa kutekeleza mpango wako, rudi, angalia ulipoteleza ili urekebishe na siyo kuufuta kabisa mpango mzima bila sababu za msingi.
Kitu kingine ni kuwa na mtandao. Mtandao ni kama daraja au miundombinu ya kuyafikia mafanikio. Hakikisha hujifungii kwenye dunia yako peke yako. Hakikisha kila unayekutana naye na kupata nafasi ya kumfahamu kama mtu anayeweza kuwa sehemu ya daraja bora kwa namna moja au nyingine, anakuwa sehemu ya mtandao wako.
Lakini kuwa na mtandao wa watu pekee hautoshi kama hautawasiliana nao. Kuwasiliana na mtandao huo ni kuufanya uwe ‘active’ ili isionekane kama unawatafuta wakati ukiwa na shida tu. Unapaswa kujipima kwa kuangalia watu wangapi wanakufahamu wewe zaidi ya watu wangapi unaowafahamu. Kwa mfano; wewe unamfahamu mkurugenzi wa kampuni ‘A’, jiulize, je, yeye anakufahamu? Kama hakufahamu, basi yeye siyo sehemu ya mtandao wako.
Lakini pia, angalia mawasiliano yako ya siku, wangapi umeongea nao kuhusu wazo la biashara au kazi?
Baada ya kuwa na hayo yote, usisahau kuwa mwaminifu. Kumbuka uaminifu utaimarisha mtandao wako kwa hali ya juu zaidi na utatafutwa kwa kuwa wewe utakuwa sehemu ya sababu ya mafanikio ya watu wengine. Kwa mfano, angalia namba ulizonazo kwenye simu yako ya mkononi. Je, ukitaka kumpigia simu dereva teksi au Bajaj au bodaboda majira ya usiku au hata muda wa kawaida utatumia vigezo gani? Bila shaka uaminifu na ukweli vitatangulia zaidi.
Kuwa mwaminifu na mkweli kwa kila mtu utakayefanya naye kazi, biashara au hata wakati mnafanya mambo ya kawaida ya kijamii kunakupa nafasi ya kuwa chaguo la kwanza kwa watu wanapohitaji huduma, bidhaa au rasilimali ambayo unayo.
Ukizingatia kwa uhakika mambo haya huku ukimkumbuka Mungu wako kwa kila jambo, utafanikiwa kweli na kubaki na amani ya moyo.
Amini katika kile unachoamini na kifanyie utafiti kujiridhisha kabla hujakubali kuyumbishwa kwa tamaa za harakaharaka ili uwe na sababu za kutosha za kukataa au kukubali jambo lolote.
Mungu akubariki, tukutane wiki ijayo!
BE INSPIRED & CHANGE
Na Eric Shigongo