×

Kigogo TAKUKURU Amwandikia Barua DPP ‘Ninakiri Nisamehe’

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Kulthum Mansoor ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amemuandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) kwa ajili ya kukiri makosa yake na kuomba asamehewe.

 

Hayo yamejili leo Jumatano, Oktoba 2, 1019 mahakamani hapo baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon kumueleza Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa bado upelelezi wa kesi haujakamilika.

 

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Utetezi, Elia Mwingira amedai kuwa mshtakiwa ameandika barua kwenda kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa, hivyo ni vyema kupata majibu kwa haraka ili mshtakiwa apate haki yake ya msingi.

 

Baada ya maelezo hayo Wakili Wankyo amedai kuwa suala hilo atalifuatilia kwa haraka zaidi. Hakimu Mhina ameahirisha shauri hilo hadi Oktoba16, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

 

Mshtakiwa Mansoor anakabiliwa na mashtaka manane ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh.Bil 1.477.