RAIS John Pombe Magufuli, amesema moja ya sababu kumtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Tafiti za Kiafya NIMR, Mwele Malecela, ni kiongozi huyo kutoa taarifa ambazo hazikuwa sahihi kuhusiana na ugonjwa wa Zika.
Magufuli ametoa kauli hiyo akiwa mkoani Songwe, wakati alipofika kwenye ziara ya kikazi na kufanikiwa kuzindua kiwanda cha kahawa kilichojengwa na wajasiriamali wa Tanzania, ambapo amesema moja ya mambo ambayo yalipelekea kumtoa kwenye nafasi hiyo Malecelea ni kutangaza ugonjwa.

“Maneno huwa hayaishi, kuna wakati walitangaza kuna ugonjwa wa Zika nchini Tanzania, alipotangaza hivyo wakati mimi najua haupo nilimfukuza saa 7:30 usiku, wala hakuna cha Zika iliyotokea. Baada ya wiki moja wakamteua akawa bosi wao, hii ilionyesha alitumwa kusema aliyoyasema; hizi ni mbinu za kibeberu,” amesema Rais Magufuli.
Kuhusiana na tukio la Mkuu wa Mkoa Mbeya kuwachapa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kiwanja mkoani, amepongeza kwa kuchukua hatua hizo kulingana na suala hilo.
“Nampongeza RC Mbeya, ila kwa wale watoto waliotimuliwa shuleni lazima wazazi wao walipe, nasema haya sio kwa sababu sina huruma, nimeshawahi kuwa mwalimu,” amesema.