MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amewarudisha makwao wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja na kuwataka kurejea shuleni hapo Oktoba 18, 2019 ambapo kila mmoja anatakiwa awe amelipa Tsh 200,000 kwa ajili ya kujenga mabweni yaliyochomwa moto.
“Kwa hiyo Mkuu wa Shule, Afande RPC, Afande OCD, sitaki kuona form five na six, wataondoka watarudi hapa tarehe 18. Na nyie form four kama kuna watu watafanya fujo, nitawatimua hata kama mitihani ni kesho, nafuta darasa zima.
“Nilipanga hapa niwatandike kwelikweli, mlambe mchanga na kokoto mmeze ili mtaje vizuri waliofanya hivyo, lakini itoshe kusema leo mtaondoka kurudi kwa baba zenu na mama zenu na mikono ikiwawasha mkachome nyumba hukohuko za baba zenu na mama zenu
“Kwa hiyo form six mko kwenye mtego, nitawafuta wote. Na hakuna mtu yoyote kuhama shule, utoke hapa uende private tuna wewe, utoke hapa uende serikalini haitawezekana, mpaka laki mbili zimeingia zimejenga mabweni.
“Mtu yeyote ambaye hataingiza pesa kabla ya tarehe 18 na kuja kuripoti shule, utafuatwa na pingu hukohuko uliko, na jambo la pili tutaku-blacklist hautafanya mitihani tena ya kidato cha sita katika maisha yako mpaka unaingia kaburini.
“Ninyi wanafunzi wote mtakuja na laki mbilimbili, na wale ambao wamekamatwa na simu mtakuja na laki tanotano na wazazi juu. Na hizo laki mbilimbili mziingize kwenye akaunti ya shule kabla ya tarehe 18 mwezi huu.
“Mliochoma Mabweni, nawaambia kama mna hamu na mnawashwa kuchoma vitu, mkachome nyumba za baba zenu. Kuanzia sasa nafunga form five na six, mnaondoka kwenda kwenu, na ikifika saa 4 bado mnang’aang’aa hapa, mtakung’utwa kichapo cha kufa mtu.
“Jana nimekuwepo hapa nimepiga watu viboko, wengine wamenijadili kwenye mitandao, Mkuu wa Mkoa anatoa wapi mamlaka haya? Eti anayeruhusiwa kupiga viboko ni mkuu wa shule. Bosi wa mkuu wa shule ni mkuu wa mkoa, mimi ndio napaswa nicharaze sana.”
Chalamila aliwacharaza bakora wanafunzi 14 wa Shule hiyo iliyopo Wilayani Chunya ambao walikutwa na simu shuleni hapo. Wanafunzi hao wanahusishwa na tukio la kuchomwa moto mabweni mawili ya shule hiyo ambayo yaliteketezwa Oktoba 1, 2019.