×

JPM: Walisema TANESCO Ubungo Haibomolewi, Nikaibomoa – Video

Rais Dk. John Magufuli leo Oktoba 5, 2019 amezindua ujenzi wa barabara ya Mpemba – Isongole iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Km 50.3 ambayo imegharimu Tsh bil 109.439, ujenzi utakamilika mwaka 2020.
Magufuli pia ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Tunduma mkoani humo na kusisitiza  wananchi kuepuka kujenga katika maeneo ya barabara, aliposema:
“Kwa mujibu wa sheria no 13 ya mwaka 2017 upana wa barabara ni mita 30 na kwa sheria ya mwaka 67 upana ulikuwa futi 22.7 kwa hiyo ukienda kujenga kandokando ya barabara unautaka umasikini na kama unataka kuwa masikini jenga karibu na barabara.
Wakati napita kwenye hii hospitali nilikuwa naiangalia hii hospitali kama ingekuwa ndani ya mita 30 ningesema ibomolewe sasa hivi lakini nikaona sheria imefuatwa. Niwaombe wananchi muendelee kufuata sheria, ukijenga kwenye hifadhi ya barabara tutabomoa tu, walisema ghorofa la TANESCO Ubungo halitabomolewa, nimeingia madarakani nimelibomoa.”

Pia alishangazwa na mwenendo mbaya wa ujenzi wa barabara ya kilomita 50 ambapo mkandarasi ametumia zaidi ya miaka mitatu bila kuukamilisha.

“Mkandarasi kutoka China anajenga kilometa 50 kwa miaka mitatu? Hii ni kwa sababu wasimamizi wetu wa Wizara wanazungumza naye kwa raha, najua waziri umenielewa.  Hizi fedha za miradi zinatoka kwa Watanzania masikini na huu ni mtego kwako. Wakandarasi wasioweza kazi msiwe mnawapa kazi,  awe ametoka China au wapi.  Pesa inayotumika hapa ni ya Watanzania masikini,  ifike mahali watu waelewe machungu ya watu hawa maskini,” alionya.

 

 

SIKILIZA HOTUBA YA RAIS MAGUFULI