



BENKI ya NBC imeendelea kuadhimisha Mwezi wa Huduma kwa Wateja kwa kufanya matukio sehemu mbalimbali nchini na hapo jijini Dar es Salaam ikitoa elimu kuhusu umuhimu wa bima na pia ikiwaleleza wateja aina mbalimbali ya huduma za bima zitolewazo na benki hiyo.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Bima wa NBC, Benjamin Nkaka alisema watanzania wanapaswa kuwa utamaduni wa kujiwekea bima wao pamoja na watoto wao dhidi ya matukio na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza wakati wowote.
Akitoa mfano wa bima hizo ni bima ya elimu ya Educare itolewayo na inayomuwezesha mzazi kuweka akiba kidogokidogo kwa ajili ya elimu ya mtoto wake pindi yatokeapo majanga yanayoweza kusababisha ulemavu wa kudumu ama kifo.
“Tumekwishakuwa na huduma hii, tunachotaka sasa ni kwa wateja kuweza kuielewa vivuri, na ndio maana tumendaa hafla kama hii ili kuwafahamisha wateja wetu na wananchi kwa ujumla huduma ya bima ya elimu ya NBC inavyoweza kumkomboa mteja,” alisema.
Alisema kwa kupitia huduma hii mteja humwekea akiba mtoto wake kidogokidogo kwa kiasi atakachopanga kwa mkataba wa muda kuanzia miaka saba hadi 18 ili kugharamia elimu ya mtoto wake.
“Bima hii ya elimu ni mpango ambao mzazi huweka akiba kila mwezi hivyo kuleta faraja moyoni kwamba endapo chochote kitatokea iwe ulemavu wa kudumu ama kifo kabla ya muda huo basi bima itagharamia elimu ya mtoto wako.
“Kiwango cha chini ni miaka saba hadi 18 na kiwango cha chini cha kuwekeza katika mpango huu kwa mwezi ni shs 7,500/- hakuna kiwango cha mwisho cha juu. Uwekezeji katika elimu ya mtoto ni jambo pekee katika kuhakikisha malengo ya kielimu ya mtoto yanatimia ,” aliongeza Bwana Nkaka.