KIJANA mmoja aliyetambulikana kwa jina la Noel Jengeni Mlilo mwenye umri 27, mkazi wa Shehia ya Wawi Wilaya ya Chakechake, na mwenyeji wa Mkoa wa Songwe, Tanzania Bara, amekutwa kichakani akiwa amefariki, katika Shehia ya Mtuhaliwa wilaya ya Mkoani Pemba.
Kaka wa marehemu, Devista Jengeni Mlilo (30), alisema marehemu aliondoka nyumbani tangu Oktoba 12, mwaka huu, na hakurudi ndipo walipoomba msaada wa polisi kwa ajili ya kumtafuta.
Aidha, amesema marehemu hakuwa na matatizo yoyote ya akili wala kiafya na alikuwa akifanya biashara zake katika maeneo ya Mkoani.
Marehemu alikuwa na majeraha madogo sehemu ya mbele ya mwili na mgongoni alikuwa na jeraha ambalo linaonyesha kusababishwa na kitu chenye ncha kali ambayo inadhaniwa kuwa moja ya sababu ya kifo chake.
Pia, mwili wake ulionyesha hali ya kukosa hewa na kuachana kwa mifupa ambayo ilisababishwa na kukabwa kwa makusudi ya kutenganisha kichwa na kiwiliwili.