×

Rais Magufuli Asikitishwa na Wizara ya Kilimo

Rais Dkt. John Magufuli amewataka viongozi wa Wizara ya Kilimo, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kubadilika na kuhakikisha haki za wakulima zinalindwa ipasavyo kwa kurejesha fedha zilizoibwa na kuzuia mianya yote ya wizi.

 

Magufuli ameelezea kutoridhishwa kwake na utendaji kazi wa Wizara ya Kilimo na viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao katika maeneo yao kumetokea wizi mkubwa wa fedha za wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) hali iliyosababisha wakulima wengi kuishi maisha duni.

 

Aidha, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango kutoa Tsh.Billion 40 ili kumaliza madeni yote ya wakulima wa korosho yaliyobaki baada ya Serikali kununua korosho za wakulima katika msimu wa mwaka 2018/2019.

Rais ametoa maagizo hayo jana November 01,2019 Ikulu Dar es Salaam alipokutana na Viongozi wa Wizara, Mikoa, Wilaya na Taasisi za Serikali ambazo zinahusika na uzalishaji na mauzo ya korosho, Mkutano huo umehudhuriwa pia na Waziri Mkuu Majaliwa.

 

“Nimesikitika kuona Viongozi wa Wizara, Mikoa na Wilaya hawajachukua hatua madhubuti dhidi ya watu wanaowaibia wakulima, mpaka nimeamua kumtuma Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brig. Mbungo ambaye kwa muda mfupi amebaini wizi wa Tsh. Billion 1.23 na tayari amefanikisha kurejeshwa kwa Tsh.Million 375 katika Mkoa wa Lindi pekee.

“Nataka mfanye kazi, hakuna wa kuwanyanyasa, nendeni mkashughulikie kero za wakulima, mna vyombo vya ulinzi na usalama nendeni mkavisimamie, kinyume na hapo nitakuona hutoshi kwenye nafasi hiyo,” amesema Rais Magufuli.