
KIJANA yupi tena wa Kitanzania anaweza asiamini kwamba anaweza kuwa sehemu ya Waafrika waliofanikiwa kimaisha kama atakuwa ni mchapakazi?
Kama yupo, basi hataki tu au ameamua kutomfuatilia kwa ukaribu Mohammed Dewji, kijana wa Kitanzania kutoka katika mji wa Singida, Katikati ya nchi ya Tanzania ambaye sasa ni gumzo katika biashara na michezo Afrika na duniani.
Watanzania wengi wanamtambua kutokana na mafanikio makubwa ambayo ameipatia Simba. Ikumbukwe ndiye alikuwa kiongozi mkuu mwaka 2003, Simba ikiwavua ubingwa wa Afrika Zamalek, kwao jijini Cairo nchini Misri, ikawa rekodi ISIYOFUTIKA MILELE.

Baada ya kurejea katika soka, Simba imekuwa tishio Afrika na ndio klabu tegemeo katika soka la Afrika Mashariki ikiwa ndani ya 10 Bora ya timu bora, maarufu katika Bara la Afrika. Huyu ni Mohammed Dewji maarufu kama Mo Dewji.
Muda mfupi tu, tokea aliporejea Simba mwaka 2017, aliifanya Simba kuwa tishio tena ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo, makombe matatu ya Kombe la Shirikisho Tanzania, ubingwa mara nne Ngao ya Jamii, bingwa Kombe la Muungano. Alipokaa kando kutokana na kubanwa majukumu, Simba ikaanza kuyumba. Amerejea tena na Simba, ndani ya muda mfupi jambo halikutegewa, Myama Simba ameanza kuamka upya na haraka sana, Tanzania na Afrika.
Kumbuka ndiye aliyeinua kwa kiwango cha juu thamani ya wachezaji wa Kitanzania na wageni katika soko la usajili na sasa timu za Tanzania zinasikika na kuheshimika Afrika nzima.
Jarida la Forbes (2025) limemtaja Mo Dewji, kuwa miongoni mwa watu matajiri duniani, akiwa na utajiri wa dola bilioni 2.2 ( zaidi ya trilioni Tsh 5.8). Mo, anakuwa tajiri namba 12 Afrika, ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki.

Orodha ya Forbes ya matajiri wa Afrika kwa mwaka 2024 ilibainisha kuwa utajiri wa Mo Dewji umeongezeka kutoka dola bilioni 1.5 hadi bilioni 1.8. Orodha ya mwaka huu inaonyesha utajiri wa Mo Dewji umeongezeka na kufikia, dola bilioni 2.2. Kwa sasa kampuni yake ya Mohammed Enterprises Ltd, ndio kampuni iliyotoa ajira nyingi zaidi kwa Watanzania.
Maana yake, Mo Dewji, shabiki lialia wa Simba, mpenda soka na maendeleo ya mchezo huu amekuwa akipanda kwa kasi, jambo linaloonyesha anafanya kazi zake kwa ubora wa juu kuendelea kukua. Kwanini vijana wengine wa Kitanzania washindwe?
Mmiliki wa kampuni ya Dangote kutoka Nigeria, Aliko Dangote kutoka Nigeria, ameshika nafasi ya kwanza katika orodha hiyo ukiwa ni mwaka wa 14 mfululizo akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 23.9, ikilinganishwa na Dola za Marekani Bilioni 13.9 mwaka jana.

Katika orodha hiyo, raia wa Afrika Kusini, Johann Rupert, anakamata nafasi ya pili akiwa na utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 14, sawa na ongezeko la asilimia 39. Anafuatiwa na mfanyabiashara wa Afrika Kusini, Nicky Oppenheimer na familia yake, wanaokamata nafasi ya tatu kwa Dola za Marekani Bilioni 10.4.
Mo Dewji kupitia MoDewji Foundation (MDF), imeshirikiana na serikali kupitia Wizara ya Maji, kuchimba visima, kukarabati na kutibu maji mkakati uliosaidia watu zaidi ya 15,000 kupata maji salama ya kunywa. Mwaka 2023 pekee, taasisi hiyo ilichimba visima 18 na kukarabati vingine vinne, hivyo kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii za vijijini unakuwa endelevu.
MDF inatarajia kuchimba visima 50 zaidi na kukarabati vingine 50 na kunufaisha Watanzania 15,000 zaidi.
Kumbuka Mo Dewji alikuwa Mbunge wa Singida mjini kuanzia mwaka 2005 hadi 2015. Wakati huo aliboresha upatikanaji wa maji safi kutoka asilimia 27-28 hadi 86-88.
Mo Dewji ni tunu kwa vijana wa Kitanzania kuanzia katika michezo ya maisha ya kawaida. Kwa wanamfuatilia na wanaotaka kujifunza kwake wanaweza kuepuka kukata tamaa, wanaweza kuepuka kuona wameshindwa kwa kuwa INAWEZEKANA.

ORODHA YA MATAJIRI WENGINE AFRIKA:
Orodha ya mabilionea wengine wa Africa na thamani ya utajiri wao kwenye mabano ni: Nassef Sawiris kutoka Misri ($9.6 bilioni), Mike Adenuga kutoka Nigeria ($6.8 bilioni), Abdulsamad Rabiu wa Nigeria ($5.1 bilioni), Naguib Sawiris kutoka Misri ($5 bilioni), na Koos Bekker kutoka Afrika Kusini ($3.4 bilioni).
