NDEGE nyingine ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Bombadier ambayo ilikuwa ikijiandaa kuja Tanzania imekamatwa nchini Canada, ambapo aliyefanya hivyo ni yuleyule (Hermanus Steyn, raia wa Afrika Kusini) ambaye aliikamata ndege kama hiyo nchini Afrika Kusini miezi michache iliyopita lakini Serikali ya Tanzania ikamshinda mahakamani.
Hayo yamesemwa leo, Jumamosi Novemba 23, 2019 na Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, wakati akihutubia baada ya Rais John Magufuli kuwaapisha mabalozi wateule watano watakaoiwakilisha Tanzania nchi mbalimbali ambapo hafla hiyo ya imefanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
“Mheshimiwa rais naomba nikupongeze kutokana na juhudi zako za kuleta maendeleo, lakini mabeberu wamekuwa wakituletea hujuma za wazi za kukurudisha nyuma.
“Jana nimemuita Balozi wa Canada, nimeongea naye kinagaubaga na kumwambia, haturidhishwi na tumechukizwa na tabia inayoendelea ya ndege zetu kukamatwa kila zinapotaka kutoka Canada, Mheshimiwa rais tunafikiri kukushauri kuhusu suala la kununua ndege Canada, si wao pekee wanaotengeneza ndege, hata Brazil wanatengeneza.
“Wanasingizia hali ya hewa, wanasimamisha safari zake, kisha wanaikamata. Kule Afrika Kusini tulimshinda kesi ya msingi na rufaa sasa hivi amekimbilia Canada, tayari tumeshapata wanasheria kule Canada na taratibu zote za kutetea ndege yetu zimeanza.
“Hoja yetu kubwa ni kuwaeleza watu wa Canada kwamba amekenda kwenye mahakama za nje ameshindwa na sasa amekimbilia Canada. Sasa tumeelewa kuwa kila unapoleta maendeleo wapo mabeberu wa nje na wengine wa ndani wanaotuhujumu. Wanakesha wakiunguruma ili wairarue nchi hii,” amesema Prof. Kabudi.
Ndege ya ATCL aina ya Airbus 200-300 ilizuiwa nchini Afrika Kusini, Agosti 23, 2019, kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg, nchini humo baada ya mkulima Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya Dola milioni 33 lakini baadaye Serikali ya Tanzania ilishinda kesi hiyo na ndege ikarejea Tanzania.