NDUGU zangu, baada ya wiki iliyopita kueleza siri ya namna ya kupata utajiri, leo nitakupa njia nyingine ambazo zinaweza kukuwezesha kuwa tajiri;
MOJA
Unaweza kurithi mali na fedha kutoka kwa wazazi wako. Hii ni njia ya kubahatisha kwani watu matajiri siyo wengi hivyo watoto wenye bahati kama hii ni wachache mno.
MBILI
Unaweza kusomea ujuzi au utaalam katika fani yenye malipo mazuri na kujiajiri mwenyewe. Kwa mfano, unaweza kusomea fani kama ya uanasheria, uhasibu na udaktari au ufundi au sanaa na kadhalika.
TATU
Unaweza kuanzisha biashara yako na kuiendesha ili kupata ziada kubwa.
NNE
Unaweza kuendeleza vipaji vyako na kuwa mwanamichezo au msanii mkubwa wa kulipwa.
TANO
Unaweza kutunga vitabu juu ya suala lolote unalolijua. Kwa mfano, kama wewe ni mtu uliyebobea katika masuala ya muziki, unaweza kutunga kitabu kinachofundisha watu namna ya kuwa mwanamuziki mkubwa duniani. Watunzi wengi wa vitabu ni matajiri wakubwa. Hii ni kazi unayoweza kuifanya mara moja, lakini ukavuna matunda yake kwa muda mrefu sana.
Unaweza kuwa mbunifu na kuanza kuuza mawazo yako au kutumia chombo ulichokibuni kukuingizia fedha.
SABA
Unaweza kucheza bahati nasibu na kushinda. Hiki ni kitu cha kubahatisha.
Inawezekana kuwa tofauti kati ya mtu tajiri na mtu maskini inatokana na kile tulichojifunza kutoka kwa wazazi wetu. Wazazi maskini huwaambia watoto wao wajitahidi kusoma sana ili wapate maksi nzuri darasani na ili baadaye waweze kupata kazi nzuri.
Wakati wazazi matajiri huwapa watoto wao elimu ya namna ya kutafuta fedha. Kwa kawaida tukiwa shuleni tunapewa ripoti ya masomo. Katika maisha tunatakiwa kuwa na ripoti yetu ya maisha nayo ni orodha ya mali tulizonazo ikiwa ni pamoja na elimu ya kuzaliwa na ya kusomea na fedha taslimu zile zilizo katika hifadhi mbalimbali.
Kwa kufuata tafsiri ya Umoja wa Mataifa, mtu maskini ni yule ambaye kipato chake hakizidi shilingi 1,000 kwa siku.
Inawezekana kuwa mfumo wa kifedha wa mtu maskini ni mfumo ambao humfanya kutumia kipato chake chote kulipia matumizi, huwa hana ziada wala uwezo wa kuweka akiba hana madeni na hana mali.
Mfumo wa fedha wa mtu mwenye kipato cha kati ni mfumo ambao humfanya kuwa na mali kama magari, nyumba na kadhalika. Mara nyingi mali hizo huwa zinapatikana kwa mikopo na hutumia mshahara kulipia matumizi na madeni, hasa kama madeni ni makubwa, mtu mwenye kipato cha kati anapaswa kumuona mshauri wa masuala ya biashara.
Hatua anazoweza kuchukua ili kujikwamua na tatizo la madeni anaweza kulazimika kuuza baadhi ya mali zake ambazo amezinunua kwa kutaka kuonesha ufahari tu na ambazo hazina umuhimu. Kwa mfano kama mtu ana magari matatu ya kutembelea, anaweza kuuza magari mawili na kubaki na gari moja na fedha atakayoiokoa kuiwekeza au kutumia kama mtaji na kuanzisha biashara ili kujiongezea kipato.
Mfumo wa mtu tajiri ni mfumo ambao unamwezesha kuwa na biashara yake, kumiliki mali nyingi, kuwa na fedha nyingi katika akiba na awe ameziwekeza kwenye vitega uchumi vinavyolipa faida kubwa zaidi ya asilimia kumi, kama vile nyumba za kupangisha na hisa.
Mtu huyu hana wasiwasi na maisha. Anaweza kusafiri au kuugua, lakini vitega uchumi vyake vinaendelea kumwingizia fedha. Siri kubwa ya matajiri ni uwezo wa kutumia fedha na kuziwekeza kupata faida kubwa.
Yote unayoyasoma hapa inabidi uyafanyie kazi ili yakusaidie. Tofauti kati ya maskini na tajiri iko katika kuchukua hatua. Tajiri hujifunza mambo ya kumwendeleza na kuchukua hatua kwa kutekeleza kwa vitendo yale anayojifunza na anayoyaona yanaweza kumuinua kiuchumi.
Maskini huwa anajifunza mambo na kuyaacha kichwani bila kuchukua hatua au kuyafanyia kazi aliyojifunza na hivyo fursa ya kupata utajiri inampita hivihivi. Kwa hiyo, kama unataka kuwa tajiri, anza mara moja kufanya yafuatayo;
Anza kuweka akiba ya shilingi 1,000 kila siku. Tengeneza kisanduku na tumbukiza shilingi 1,000 kila siku. Zikifika shilingi 50,000, kafungue akaunti. Kisha endelea kuweka 30,000 kila mwezi. Jinsi mapato yako yatakavyokuwa yanaongezeka, tenga asilimia kumi (10%) ya mapato yako uweke akiba kila mwezi.
Lengo lako liwe ni kuweka 10,000 au zaidi kila mwezi. Fedha unayoweka ni kama unapanda mbegu.
hii ndiyo hatua ya kwanza kuelekea kwenye utajiri.
Fedha utakazoziweka usiziguse mpaka ukiona zimekuwa nyingi ndipo utaamua na kupanga ukaziwekeze sehemu gani.
MBILI
Jifunze pia mbinu za kutafuta fedha. Njia rahisi ni ya uhakika ya kukuwezesha kufanikiwa kiuchumi katika maisha ni kutafuta mshauri au mtaalam anayejua mbinu za uongozi wa biashara ili akushauri vizuri juu ya yale unayonuia kutekeleza.
TATU
Inawezekana pia bado hujawa na biashara ya aina yoyote. Kama ndivyo anza kufanya utafiti kuona utafanya biashara gani. Nimekwishaeleza hapa jinsi ya kupata wazo la biashara. Kumbuka kwamba kuwa na biashara yako ni siri ya pili ya kuelekea kwenye kupata utajiri.
Kama unayo biashara yako unaweza kumtafuta mtaalam wa biashara kuangalia jinsi unavyoweza kuiboresha au kuipanua.
NNE
Panga malengo ya muda wa mwaka mmoja, miaka mitano na miaka ishirini kama Mungu atakujalia uhai ili kuhakikisha kwamba unajikomboa kiuchumi. Malengo yako makuu yawe ni; kuwa na akiba ya fedha za kutosha katika akaunti yako, kuwa na biashara yako na vitega uchumi vya aina tofauti ambavyo unaweza kuvisimamia vizuri.
Kama wewe ni mwajiriwa, kipimo chako cha mafanikio kiwe ni kujiuliza swali, kama utaacha kazi yako ya mshahara utaweza kuishi kwa kutumia kipato chako cha pembeni kwenye biashara yako kwa muda gani?
Mafanikio yako yatakuja pale utakapoweza kutumia kipato chako cha ziada bila kutegemea mshahara na hapo ndipo unaweza kuacha kazi na kwenda kuimarisha biashara zako au kuendelea na kazi huku pia ukijiimarisha kibiashara.
SITA
Kama utafuata mpango wa namna hii na kujituma kwa juhudi na maarifa kwa muda wa miaka mitano (5) unaweza kuwa tajiri na maisha yako yanaweza kuwa mazuri.
Mungu akubariki, tukutane wiki ijayo.
BE INSPIRED & CHANGE