ESTER Kiama, mrembo kutoka Bongo Muvi, ameamua kutunisha msuli wa kifedha na kuteketeza mamilioni ili kwenda sambamba na msanii mwenzake, Aunt Ezekiel ambaye amemtangulia kwa kumiliki pub yake maeneo ya Mikocheni jijini Dar.
Mrembo huyo, amefungua pub yake inayokwenda kwa jina la The Joint maeneo ya Mikocheni ambapo taarifa zinaeleza kuwa ameteketeza si chini ya shilingi milioni 20 na alitarajia kuizindua siku ya Ijumaa iliyopita.
“Kajitutumua kweli, eneo lile ni la gharama kidogo kuanzia kukodi kupapamba jinsi anavyotaka na vinywaji alivyonunua, siyo chini ya milioni 20 ametumia, sasa atakuwa sawa na Aunt,” kilieleza chanzo chetu makini.
Baada ya kupenyezewa ubuyu, Risasi Jumamosi lilimtafuta Ester ambapo alikiri kufungua pub hiyo lakini akasema hajamjibu mtu bali amefanya kwa manufaa yake.