
TANGU msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’, aanze kuwika akiwa ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), hajawahi kuwa sehemu ya kupanda kwenye jukwaa la Tamasha la Fiesta.
Miaka ya nyuma kabla hajatoka kimuziki, Harmonize aliwahi kuomba kupanda kwenye jukwaa la Fiesta mkoani Mtwara, akapata nafasi ya kutumbuiza kwenye shoo za utangulizi. Cha ajabu hakuweza kubahatika kuigusa steji ya Fiesta kufuatia kukumbwa na msala wa vibaka akiwa njiani kwenda kutimiza lake la kupiga shoo, akaibiwa kila kitu.
Harmonize anasema siku hiyo ilikuwa ngumu sana katika maisha yake kwani baada ya tukio hilo, aliamua kurudi katika nyumba ya wageni aliyofikia akiwa amechanganyikiwa kutokana na kuibiwa kila kitu zikiwemo fedha ambazo alipanga kufanya nauli ya kurudia jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, aliweka wazi kuwa, changamoto hiyo ilimfanya kukaa chini na kufikiria kwa kina kisha akaamua kuchukua nguo zake na kuziuza kwa lengo la kufanikisha safari ya kurejea Dar es Salaam. Kabla ya kuanza safari hiyo, ilimlazimu kumtafuta mmoja wa watangazaji wa redio mkoani Mtwara na kumuomba namba ya Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ili akifika tu Dar amuombe kujiunga naye.
Hilo kwake likafanikiwa, alipofika Dar es Salaam, alimtafuta Diamond kwa lengo la kumuomba aweze kumsaidia kimuziki, ombi lake lilifanikiwa. Anasema kwamba hakuamini jinsi alivyojibiwa na Diamond ombi lake hilo la kumsaidia, kisha akaanza kuishi naye nyumbani kwake na baadaye kumvusha kimuziki.

Hivi sasa Harmonize hayupo WCB baada ya kutoka na kuamua kufanya kazi zake mwenyewe, sasa kwa mara ya kwanza leo Jumapili, atapanda kwenye JukwaalaFiesta pale Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Hii itakuwa historia kwake kwani wakati ule hakuwahi kufanikiwa kutimiza lengo lake la kupanda jukwaani, lakini safari hii kama mambo yakienda sawa, Mungu akimpa afya njema, atatimiza lengo lake hilo. Harmonize anatarajiwa kuliongoza jahazi la burundani katika Jukwaa la Fiesta ‘Levels Baby’ akiwa na wakongwe wengi akiwemo Alikiba, Jay Moe, Chege, Juma Nature, TID na Profesa Jay.
Uwepo wa Harmonize leo, kunawafanya wengi kusubiri kwa hamu kuona atafanya nini kwenye tamasha hilo ambalo kiingilio chake ni shilingi 3,000 tu (shilingi elfu tatu) kwani itakuwa ni shoo yake ya historia.
Harmonize kwa sasa anatikisa na Wimbo wa Uno, aliouachia siku chache tu baada ya kujiengua WCB. Mbali na Uno, hivi karibuni ametoa ngoma nyingine iitwayo Kushoto Kulia, ambayo kwa namna fulani imezua gumzo kubwa kufuatia namna video yake ilivyoandaliwa.
Wasanii wengine ambao wanatarajia kuwepo katika tamasha hilo ni Aslay, Rostam, Janjaro, Maua Sama, Billnass, Wini, Country Boy, Shilole, Fid Q, Young Dee, The Mafik, Marioo, Mr Blue, Barnaba, Ruby, One The Incredible, Jay Melody, Meja Kunta, Isha Mashauzi, Young Lunya, Fany, Nandy, Rich Mavoko, Weusi, Nay Wa Mitego, Goodluck Gozbert, Mimi Mars, Baddest47, Nedy Music, Sholo Mwamba, Benson, Mzee wa Bwax na Ras Gwandumi.
STORI NA MUSA MATEJA | GPL