×

Mo Dewji Awajia Juu Mapro Wa Simba, Afunguka Alivyolia

Klabu ya Simba, leo Desemba 8, 2019 wanafanya Mkutano Mkuu wa mwaka 2019  kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) abapo mgeni rasmi ni Naibu Spika, Dkt.Tulia Ackson.  Katika mkutano huo Mfanyabiashara maarufu nchini ambaye pia ni mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo akizungumza na wanachama wa klabu hiyo amesikitishwa na nidhamu mbovu ya baadhi ya wachezaji nje ya uwanja pamoja na  kitendo cha kutolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alichokisema Mohammed Dewji ‘Mo;-
“Leo nianze na neno moja kubwa na lenye maana pana sana, Alhamdulillah! Shukrani za dhati ziende kwa Mungu wetu Mtukufu kwa hapa tulipo! Hakika hizi ndio ndoto zetu wanasimba wote, kuifikisha klabu yetu kwenye kilele cha mafanikio.
“Jana Jumamosi yalitimia kule Bunju, na leo tupo hapa na wanachama wenzangu kujadili mustakabali wa klabu yetu, tena kwa amani na utulivu mkubwa, hizi ndio ndoto zetu.
“Mnafahamu kwa sasa mchakato wa kubadilisha muundo wa klabu yetu umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90, na yamebaki mambo machache muhimu ili sasa Simba iwe kampuni kamili, itakayoendeshwa vile Wanasimba mlivyotaka.
“Jana tuliwaonyesha uwanja wetu wa mazoezi ambapo kutakuwa na viwanja vizuri na vya kisasa, cha nyasi bandia na majani asilia, pamoja na viwanja hivyo tumejenga chumba cha kubadilishia nguo chenye ubora na fensi ya kulizunguka eneo la viwanja.
“Hii ni awamu ya kwanza, yanayokuja pale Bunju Complex yatafurahisha nchi na Wanasimba wote, katika suala la miundombinu ya Bunju niwahakikishie wanachama wenzangu mambo yatakuwa bul bul.
“Awamu ya pili ya ujenzi wa Bunju Complex, kujenga hosteli yenye vyumba vya kulala, gym, ofisi za benchi la ufundi, jiko na kantini ya chakula, nutritional center, chumba maalum cha kitaalam kwa uchambuzi wa mechi zetu na mazoezi, pamoja na technical room.
“Mradi huu unatarajiwa kuwa na thamani ya Tsh. Bilioni 2.5 na kwa kuanzia kama mwanachama na Mwenyekiti wa Bodi nitachangia kiasi cha Tsh. milioni 500. Wanasimba wanahamu ya kuchangia ujenzi na upanuzi wa Bunju Complex.
“Kiasi kilichobaki tutafanya fund rising ili kupata fedha inayotakiwa, bila shaka tutafanikiwa ili kwenye msimu wa 2021/22 tuwe kwenye hostel zetu. Kazi yangu ni kuhakikisha wachezaji wanapata mazingira bora na mishahara mizuri ili waweze kufocus na kushinda.
“Tuna mpango wa kufungua Simba Academy ili hapo baadaye tuje kuvuna vijana waliolelewa kwenye asili ya Simba. Tuwafundishe vijana hao thamani ya Simba na falsafa ya uchezaji wa Simba, na sambamba upendo ili wawe na uchungu zaidi na klabu yetu.

“Msimu uliopita ulikuwa mzuri sana kwetu kwa ujumla wake. Kucheza hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kisha kuvuka hadi robo fainali ilikuwa ni jambo kubwa kwa klabu, ukizingatia pia tuliweza kutetea ubingwa wetu wa nchi.

 

“Kuzifunga nyumbani klabu kubwa kama Mbabane, Nkana, Soura, Ahly na AS Vita ilikuwa ni heshima kubwa. Hususani tulikuwa tukiwafunga mbele ya mashabiki wetu 60,000 waliokuwa wakituunga mkono kwa hali na mali. Binafsi msimu uliopita ulikuwa amazing.
“Niliumia sana kupoteza mechi iliyoandaliwa na wadhamini wetu SportPesa, ambayo tulicheza na klabu kubwa ya Sevilla kutoka Hispania. Ile mechi tulikuwa tushaongoza kwa idadi nzuri ya magoli, lakini kilichotokea hadi sasa sielewi, lakini ndio football ilivyo.
“Tulipata shida kidogo katika msimu huu. Nikisema ni bahati mbaya ni utetezi dhaifu, itoshe kusema yaliyotokea msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni fundisho kuu kwetu, na nadhani hatupaswi kurudia makosa tuliyoyafanya. Ilikuwa ni aibu kwetu, na tulijiangusha.
“Binafsi bado sijakaa sawa hadi leo baada ya matokeo ya mechi yetu dhidi ya timu ya UD Songo. Nilikuwa sipo nchini. Baada ya mechi ile kuisha, nililia mnoo.
“Iliniumiza kupita maelezo. Lakini tumefundishwa katika soka kukubali matokeo yote matatu, ingawa mimi nataka klabu hii, iwekeze katika tokeo moja tu, la ushindi! .
“Siridhishwi hata tone na nidhamu ya baadhi ya wachezaji wetu nje ya uwanja. Nimekuwa mnyonge kuona uwekezaji tuliouweka kwao, baadhi yao, huutumia kama fimbo ya kutuchapia.
“Niwaambie wachezaji wote, Simba ni klabu kubwa kweli kweli, tena kubwa hasa, na hakuna shaka ni namba moja Afrika Mashariki, bodi ninayoiongoza mimi haitavumilia mchezaji yoyote asiyejua thamani ya Simba. Kuonyana onyana sasa imetosha.
“Sisi tunawalipa vizuri mno, na wao wana wajibu wa kutulipa matokeo na furaha. Na ili furaha iwepo, lazima nidhamu isimamiwe kikamilifu, na katika hili hatutanii. Hatutajali ukubwa wa jina la mchezaji yoyote.
“Nidhamu kwetu ni muhimu kama tunataka tufikie malengo tuliyokusudia. Na haya ndio yaliyotufanya bodi tuchukue maamuzi magumu kwa kocha wetu. Timu imeshindwa kufikia malengo, kisha nidhamu hakuna, alafu tuvumilie?
“Simba lazima tuamue kuteseka na moja katika mambo haya mawili, (1) tuzoee uchungu na maumivu ya nidhamu au (2) maumivu ya matokeo mabaya. Kama mpenzi wa Simba, siwezi.
“Klabu yetu imeimarisha sana timu zake za vijana na wanawake, na sasa sisi ni miongoni mwa klabu chache Tanzania zenye timu imara za vijana chini ya miaka 20, na ile ya miaka 17, na tuna timu nzuri ya wanawake, na tunazidi kuziimarisha.
“Na katika msimu huu wa ligi, tutahakikisha tunachukua tena ubingwa ili tuje kuweka rekodi nyingine kwenye klabu bigwa Afrika. Nawahakikishia wanachama wenzangu kujikwaa si kuanguka, hatutarudia makosa! Insha’Allah, Mungu atutangulie.
“Wiki hii, tunaleta kocha mpya, kocha mwenye kiwango kinachostahili kufundisha mabingwa wa nchi hii. Sasa tunaleta kifaa. Mtatangaziwa rasmi, ni nani, na anatoka nchi gani.
“Baada ya kusema hayo napenda kuishukuru Bodi ya Wakurugenzi ninayofanya nayo kazi. Hawa ni watu makini na wananisaidia sana katika kutimiza wajibu wangu, kama mwenyekiti wao na mwekezaji ndani ya klabu hii.

“Kipekee, niishukuru kwa dhati serikali yetu chini ya Mhe. Rais Dkt. John Magufuli, hakika serikali hii inatupa kila ushirikiano tunaohitaji kama klabu. Nimshukuru Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

 

“Niseme kitu kuhusu mgeni rasmi wetu wa leo, Naibu Spika. Amedhihirisha Usimba wake wa kindakindaki. Alfajiri ya leo alikuwa anaongoza msafara wa wabunge wenzike kwenda Uganda, lakini amehairisha safari hiyo muhimu baada ya kupokea mwaliko wetu.”

Leave a Comment