
MKUU wa Wilaya ya Geita, (DC) Josephat Maganga (pichani) amesema mojawapo ya sababu iliyomlazimu kumsweka rumande askari wa usalama barabarani, WP 10086 PC Doto Kisiri ni kuwafunza na kuwakumbusha umuhimu wa kuwa na nidhamu askari wa aina hiyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya mkuu huyo wa wilaya, kumuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, SSP Sindano kumuweka mahabusu kwa zaidi ya siku mbili, askari huyo wa usalama barabarani kwa kosa la kutompigia saluti.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA hivi karibuni, DC Maganga alisema suala hilo ni la kiulinzi, kiserikali na linahusu nidhamu ya utumishi.
Alisema suala la kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari ni utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa yeye ndiye kiongozi wao.
“Kwa sababu mwanafunzi akikosea darasani kama vile akipigana na mwenzie, anaweza kuchapwa na mwalimu, mimi ndiye kiongozi wa huyo mtu.
“Kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya polisi ni utekelezaji wa kazi zetu, haya mambo mengine hutakiwi kuandika kuwa mkuu wa wilaya kamweka ndani, andikeni matukio kama simba kamla mtu kwa sababu haya ni masuala ya kinidhamu,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ACP Mponjoli Mwabulambo alisema masuala ya kinidhamu ni jambo la kawaida ndani ya jeshi hilo kwa kuwa ni taasisi.
“Najaribu kufikiria unaingia kwenye eneo hilo kwa sababu gani wakati jamii haikuathirika na lolote?
“Mambo mengine ni ya kitaasisi, ni vya kijeshi mno, watu wanalichukulia jeshi la polisi kama la watu wa kawaida hivi,” alisema.
Hata hivyo, Gazeti la IJUMAA lilimtafuta bila mafanikioni askari huyo kwa njia ya simu ili afafanue zaidi kuhusu hatua alizochukuliwa.
Aidha, kwa mujibu wa chanzo chetu mkoani humo, pia imeelezwa kuwa askari huyo amehamishwa kituo cha kazi baada ya mkuu huyo wa wilaya kudaiwa kukataa kufanya kazi na askari huyo kwa kuwa ni mtovu wa nidhamu.
TUKIO LILIVYOKUWA
Ilielezwa kuwa, Novemba, mwaka huu, askari huyo, WP Doto aliwekwa mahabusu ya polisi katika kituo kikuu cha polisi Wilaya ya Geita kwa zaidi ya saa 24 na siku chache baadaye alihamishiwa katika Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ambako anaendelea na majukumu yake.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Mwenyekiti wa Stendi Kuu ya Mabasi –Geita, Kharid Faraji alisema tukio hilo lililotokea mapema Novemba, mwaka huu, muda wa saa 2:30 asubuhi wakati askari huyo akiwa ‘bize’ kukagua magari ili kuhakikisha abiria wanasafiri salama huko waendako.
Alisema wakati askari huyo akiendelea na ukaguzi wa magari, hayo mkuu wa wilaya alipita, lakini kwa bahati mbaya hakumuona kutokana na kazi iliyokuwa mbele yake ya kuhakikisha usalama wa abiria.
“Kwa vile DC alikuwa amemuona askari huyo alimwamuru dereva wake kusimamisha gari analolitumia kisha kushuka na kurudi kwa miguu hadi eneo ambalo askari huyo alikuwa akiendelea na ukaguzi wa magari.
“Tulisikia akiwa anamuuliza askari huyo…‘Kwa nini hujanipigia saluti? Na askari alijibu ‘samahani mkuu sikukuona wakati unapita’ majibu ambayo hata hivyo, hayakuweza kumridhisha DC.
“Baadaye tuliona DC anapiga simu kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Geita aliyefika eneo la tukio bila kuchelewa,” alisema.
Aliongeza kuwa, baada ya OCD kufika, DC Maganga alimwamuru OCD amkamate askari huyo na akawekwe mahabusu mara moja kwani alionesha utovu wa nidhamu kuacha kumpigia saluti ili hali akijua yeye ndiyo Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyekuwapo siku ya tukio naye aliongeza kuwa alimsikia pia DC huyo akimwagiza OCD kuwa hataki kumwona askari huyo ndani ya wilaya yake.
“Na kweli bana, zaidi ya mwezi sasa dada wa watu hatumuoni tena hapa Geita, maana inadaiwa baada ya kukamatwa na kupelekwa kituoni sasa kilichoendelea huko kituoni hatujui,” alisema mkazi huyo ambaye alikataa kutaja jina.
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa hii ni mara ya pili kwa mkuu huyo wa wilaya kumweka mahabusu askari kwa kosa la kutopigiwa saluti.
Mapema mwaka huu, askari huyo wa usalama barabarani aliyefahamika kwa jina la PC Jackson naye aliwekwa ndani kwa kosa kama hilo japokuwa hakuhamishwa kituo cha kazi.
Stori: MWANDISHI WETU, Ijumaa