
ALIYEKUWA beki wa kushoto wa JKT Tanzania, Adeyun Saleh amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga, anakuwa mchezaji wa tatu aliyesajiliwa na timu hiyo msimu huu wa usajili wa dirisha dogo uliofunguliwa Desemba 16.
Adeyun ambaye kabla ya kusajiliwa na timu hiyo uongozi wa Yanga, ulitaka kwanza kumfanyia vipimo vya afya kwa ajili ya kumuangalia afya yake kwani mara kwa mara amekuwa akiumia na kushindwa kumaliza msimu akiwa fiti.
Mchana wa leo Jumatano, Yanga wametoa taarifa ya kumsaini Saleh kwa mkataba wa miaka miwili na kumtambulisha rasmi akiwa na Katibu wa timu hiyo, David Luhago.
Kabla ya kusaini Saleh ambaye alikuwa pendekezo la kwanza la kocha wa muda wa Yanga Boniface Mkwasa, alikuwepo beki mwingine wa kushoto Yassin Abdallah, kutoka Polisi Tanzania ambaye alikuwa chaguo la pili.
Yanga mbali ya kumsaini Saleh tayari wamewasainisha Ditram Nchimbi, Tariq Kiakala kutokea Misri huku kukiwa na taarifa za kumnasa pia anatajwa kiungo Haruna Niyonzima kutokea AS Kigali ya Rwanda na Luis Miquissone kutoka UD Songo ya Msumbiji.