
MGOMBEA wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amechaguliwa tena katika nafasi hiyo baada ya kupata kura 886 sawa na 93.5% dhidi ya mpinzani wake Cecil Mwambe aliyepata kura 59 sawa na 6.2%. Mbowe atatumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Matokeo hayo yametangazwa leo Alhamisi, Desemba 19, 2019, saa 11 alfajiri na msimamizi wa uchaguzi, Sylvester Masinde, akibainisha kuwa kura tatu ziliharibika. Uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Baada ya Masinde kumtangaza Mbowe kuwa mshindi, idadi kubwa ya wajumbe wa mkutano mkuu walinyanyuka kwenye viti na kumfuata mbunge huyo wa Hai kwa ajili ya kumpongeza.
Wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa (Bara) walikuwa wagombea wawili, Tundu Lissu na Sophia Mwakagenda, Lissu amepata kura 930 sawa na 98.8% huku Mwakagenda (aliyetangaza kujitoa akiwa ukumbini) akipata kura 11 sawa na 1.2%.