
NI Jumamosi nyingine wewe mpenzi wa My Style tunakutana kupeana michongo mbalimbali kutoka kwa mastaa kuhusu mitindo na maisha yao kwa jumla.
Leo tupo na staa wa Bongo Fleva ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake ya Mungu Anakuona, Emmanuel Elibaliki ‘Nay wa Mitego’. Ungana naye;
My Style: Kwanza kabisa mashabiki wako wangependa kujua, ukiamka asubuhi ni jambo gani huwa ni la kwanza kulifanya?
Nay: Jambo la kwanza namshukuru Mungu kwa kuniamsha salama kisha naenda kuoga. Baada ya hapo ndiyo naendelea na mambo mengine.
My Style: Ukiwa na msongo wa mawazo huwa unapenda kufanya jambo gani ambalo unahisi ndilo hukufanya uwe sawa?
Nay: Nikiwa na mawazo huwa napenda sana kukaa na watu, yaani nikikaa na jamaa zangu ndiyo akili yangu inatulia na jambo lingine nikiwa karibu na watoto wangu, huwa mawazo yanaondoka kabisa.
My Style: Starehe yako kubwa ni nini?
Nay: Ni muziki, starehe yangu ya pili muvi, ya tatu ni mapenzi na ya nne gemu, napenda sana kucheza gemu ya PS.
My Style: Unapenda kushiriki tendo la ndoa na mwanamke wa aina gani?
Nay: Kwanza lazima watu wajue kwamba napenda mapenzi ila siyo na mtu ambaye sijampenda, mara nyingi huwa napenda kushiriki tendo la ndoa na mwanamke ambaye nina hisia naye hata nikikaa naye nafurahi, siyo ile nimejisikia tu hamu ndiyo natafuta mtu, hapana, huwa sipendi kujutia baadaye maana kuna ile unakuta mwanaume analala tu na mwanamke hata kama hajampenda halafu baadaye anaanza kujutia, sasa hicho kitu mimi ndiyo sikipendi.
My Style: Unaweza kukaa muda gani bila kushiriki tendo la ndoa?
Nay: Mimi naweza kukaa hata mwezi sijafanya hicho kitu.
My Style: Kuna wanaume ambao hawawezi kukaa hata siku tatu bila kushiriki tendo la ndoa, hilo unalionaje?
Nay: Ni kujiendekeza tu na jinsi unavyojiweka mwenyewe, lakini ukiamua unaweza kwa sababu siyo jambo gumu.
My Style: Viwanja vyako vikubwa vya starehe hapa Bongo ni vipi?
Nay: Mimi sipendi sana kutoka, labda siku nikiamua kuwatoa watoto wangu ndiyo huwa napenda kuwapeleka White Sands (Mbezi-Beach).
My Style: Ukipata nafasi ya kutulia nyumbani na familia yako huwa unapenda kufanya nini?
Nay: Mara nyingi nikiwa nyumbani huwa napenda kujua kitu gani kipo na kipi hakipo, jambo gani lipo sawa na lipi halipo sawa, yaani nyumba nzima kisha narekebisha kila kitu.
My Style: Unapenda kutoka na mpenzi wako akiwa katika muonekano gani wa mavazi?
Nay: Napenda kutoka na mpenzi wangu akiwa amevaa smati, ile ki-wife material, yaani avae ionekane nipo na mwanamke siyo mdada wa mjini ili hata tukikutana na mama Nay njiani asione noma kutusalimia.
My Style: Unaweza kutoka na mwanamke akiwa hajapaka make-up?
Nay: Mimi mwanamke anayependa kupaka make-up nyingi kwanza simpendi, sipendi mwanamke ambaye yupo complicated sana, napenda mwanamke awe simpo ndiyo anapendeza.
My Style: Rangi gani za nguo unazipenda sana?
Nay: Napenda rangi nyeupe, nyeusi na nyekundu.
My Style: Aina gani ya mavazi ambayo ukiyavaa unajiona umetokelezea zaidi?
Nay: Pensi na t-shirt, simpo yaani halafu napendeza kinyama.
My Style: Msanii gani wa kike hapa Bongo mavazi yake yanakuvutia zaidi?
Nay: Flaviana Matata.
My Style: Unatembelea gari la aina gani na lipi ni gari la ndoto yako?
Nay: Nina gari tatu za kutembelea, nina Toyota Prado, Toyota Alphad kwa ajili ya safari na nina Toyota Mark X, lakini gari la ndoto yangu ni Range Rover, Mungu akijaalia mwakani nitakuwa nalo.
My Style: Kiasi gani cha pesa ambacho Nay hawezi akakitoa kununua nguo?
Nay: Shilingi laki moja siwezi kutoa hiyo pesa kununua nguo, yaani mimi nimenunua nguo kali kinoma nimetoa shilingi 50,000 tu kwa sababu pia mimi kwenye maduka yao (maduka makubwa wanayoingia mastaa) siingiagi, mara nyingi nguo zangu watu wananipitishia mfano hizi nguo nilizovaa hapa ni shilingi 10,000 tu juu mpaka chini.
My Style: Kwa hiyo siku ukiamua kuvunja kabati juu mpaka chini huwa unatumia kiasi gani?
Nay: Yaani nikihitaji kupendeza ile kiukweliukweli juu mpaka chini, watoto wa mjini wanasema kuvunja kabati, natumia shilingi laki na nusu na hiyo nimejipiga sana.
My Style: Wewe ni ‘chizi’ wa nini hasa?
Nay: Mimi ni chizi vipensi, napenda sana.
My Style: Kwa hiyo hata mtu akikuuzia shilingi laki moja utanunua?
Nay: Nitanunua kwa sababu navipenda, lakini roho itaniuma kwa sababu bei zake nazijua ni shilingi 5,000, 7,000, 10,000 mpaka 15,000.
Makala: Memorise Richard