
SERIKALI ya Urusi imefanikiwa kufanya majaribio ya mtandao uitwao Runet, ambao ni mbadala wa mtandao wa intaneti unaotumika hivi sasa duniani.
Maelezo kuhusu nini kilifanyika katika majaribio hayo hayakuwekwa wazi, lakini kulingana na Wizara ya Mawasiliano ya nchi hiyo, watumiaji wa kawaida hawakuona tofauti yoyote.

Jaribio hilo linatafsiriwa kama mpango wa Serikali kuminya mawasiliano ya watu nchini Urusi ambapo Wataalamu bado wana wasiwasi kuhusu jinsi gani baadhi ya nchi wanaminya mawasiliano ya intaneti.
Matokeo ya zoezi kwa ujumla wake, yameonesha kuwa Serikali na makampuni ya mawasiliano yapo tayari kujibu mapigo kutokana na hatari na vitisho vinavyojitokeza ili kuhakikisha kuwa intaneti na mitandao ya ndani ya Urusi inafanya kazi katika hali yoyote ile.