×

Niyonzima Ampa Kiburi Yondani Yanga

BEKI mkongwe wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani ameusifu usajili mpya wa timu hiyo ambao anaamini utaimarisha kikosi chao katika kuelekea michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara ukiwemo dhidi ya watani wao wa jadi Simba.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Januari 4, mwakani katika mchezo wa ligi uliopangwa kupigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam uliojaa upinzani mkubwa.

 

Yanga hadi hivi sasa tayari imewasajili watano pekee katika dirisha dogo lililofunguliwa wiki iliyopita ambao ni Mnyarwanda Haruna Niyonzima, Ditram Nchimbi, Adeyum Salehe, Tariq Seif na Muivory Coast Ykiep Gnaimen.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Yondani alisema usajili huo uliofanywa na viongozi wa timu hiyo umeendana na mahitaji ya kikosi chao ikiwemo safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa tatizo kwao kupata matokeo mazuri.

Yondani alisema kuwa wachezaji wote waliosajiliwa ni wale wenye uzoefu na uwezo wa kucheza akiwemo Niyonzima ambaye anaifahamu vizuri ligi ya ndani, hivyo hana hofu naye mara atakapojiunga na timu hiyo katika kujiandaa mchezo wao dhidi ya Simba.

 

Aliongeza kuwa katika kuelekea mchezo wa watani wa jadi, hana hofu kutokana na kucheza michezo mingi iliyowakutanisha wakongwe hao Simba na Yanga.

 

“Nimefurahi usajili uliofanywa na viongozi, nianze kwa kuwapongeza kwa kuona tatizo lililokuwa linaisumbua timu na kusababisha kupata matokeo mabaya katika michezo ya ligi.

 

“Mara nyingi nimekuwa nikiumia na kukasirika pale timu inapopata matokeo mabaya kutokana na umakini mbaya wa safu ya ushambuliaji iliyokuwa inashindwa kutumia nafasi nyingi za kufunga mabao.

 

“Lakini hivi sasa sitaumia kutokana na wachezaji wengi waliosajiliwa wote kuwa na uzoefu, viwango vya kucheza ambao kati yao nawafahamu akiwemo Niyonzima, Nchimbi na Adeyum, hivyo mashabiki wajiandae kupata furaha,” alisema Yondani.

Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam

Leave a Comment