
Rais John Magufuli leo Jumapili Desemba 29, 2019 amewasilisha fomu ya tamko kuhusu Rasirimali na Madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Dar es Salaam.
Fomu hizo zimewasilisha na Katibu wake, Ngusa Samike kwa niaba ya Rais Magufuli aliyepo wilayani Chato mkoani Geita kwa mapumziko.
Akipokea fomu hizo, Kamishna wa Maadili, Jaji mstaafu Harold Nsekela amempongeza mkuu huyo wa nchi kwa hatua hiyo akisema ametekeleza matakwa ya Kikatiba na Sheria ya Maadili.
“Viongozi kurejesha tamko ni jambo la kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 132 (5)b. Ibara hii inasema msingi wa maadili wa viongozi wa umma, itawataka watu fulani walioshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo kuhusu mapato, rasirimali na madeni yao.
“Katiba ndiyo inatatuka sisi viongozi kutoa maelezo haya kila mwaka. Ukija katika sheria yetu namba 13 ya mwaka 1995 kifungu 9 inaeleza kila mwisho wa mwaka kiongozi anatakiwa kumpelekea kamishna tamko la maandishi,” amesema Jaji Nsekela.
Jaji Nsekela amempongeza Rais Magufuli kwa kurejesha tamko la mapato, madeni na rasirimali zake kama kiongozi wa umma, huku akiwataka viongozi wasiorejesha kufanya hima kutekeleza mchakato huo kwa sababu zimebaki siku mbili pekee.
“Niwakumbushe Desemba 27 mwaka 2017 wakati Rais Magufuli anarudisha tamko aliniambia ikifika Desemba 31 tuchore mstari. Nawaomba viongozi wenzangu ambao bado hawajaresha, turejeshe siyo kwa sababu Rais Magufuli amerudisha ila ni jambo la kikatiba.
“Tusifanye mzaha, kitu gani kitatokea hapo baadaye hayo ni ya kwangu kama sekretarieti. Aliyenipa hii kazi atakuja kuniuliza baada ya viongozi kurejesha matamko mimi na wenzangu tumefanya nini, ninachotaka kuhakikisha viongozi wenzangu sitaki kuwajibika, wasiorejesha kabla ya Desemba 31 sheria ipo wazi kitu gani kitatokea,” amesema.