![]()
UNAWEZA kusema kuwa ni pigo kubwa kwa klabu ya Manchester United baada ya staa waliyekuwa wakimwania kwa nguvu kubwa Erling Braut Haaland kusajiliwa na Borrusia Dortmund.
United walikuwa wamemweka staa huyo kama tageti namba moja kwenye usajili wa Januari mwaka huu lakini wanaonekana kuzidiwa ujanja.
Huyu ni mmoja kati ya wachezaji wa timu ya RB Salzburg ambaye alionyesha kiwango cha juu sana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Dortmund juzi waliwashangaza Man United baada ya kumtangaza mchezaji huyo na kuonyesha kuwa wamempa mkataba wa miaka minne.
Mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa hali ya juu atakuwa sasa akichukua mshahara wa pauni 130,000 kwenye kikosi hicho na atakaa hapo hadi mwaka 2024.
Mchezaji huyo raia wa Norway amezivutia timu kadhaa kubwa za Ulaya na anaaminika kuwa atakuwa mchezaji mahiri sana kwenye soka kwa sasa.
Dortmund wamekuwa wakifanya makubwa kwenye soka duniani na huyu anaweza kuwa mchezaji staa kwenye timu hiyo kama walivyokuwa wengine wengi ambao wamepita hapo.
Kwa mujibu wa magazeti kadhaa ya Ulaya staa huyo amesajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 18 lakini United walikuwa wanatajwa kumtaka kwa pauni milioni 25.
Hii inaonyesha aidha yeye au klabu yake hawakutaka ajiunge na United na ilionekana kuwa anaweza kuwika zaidi akiwa na Dortmund ambayo imekuwa ikifanya vizuri kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga kwa miaka kadhaa sasa.

“Kwenye moyo wangu kumekuwa na mawazo kadhaa kuwa natakiwa kuondoka kwenye klabu hii na kwenda sehemu nyingine.
Hakika nina furaha sana kwa kuwa nakwenda kwenye timu ambayo nitakuwa mbele ya mashabiki 80,000 kwenye kila mchezo.
“Hakika hili ni jambo zuri sana kwangu na nasubiri kwa hamu kubwa kuona siku hiyo inatokea.
“Sasa naona ndoto zangu zimetimia, nasubiri kwa hamu kubwa kuvaa jezi ya Dortmund msimu huu.”
Dortmund wamekuwa na historia nzuri ya kuchukua wachezaji wengi vijana na kuwafanya masupastaa ambao aidha wamekuwa wakiwasaidia wenyewe au wamekuwa wakiwauza kwa viwango vikubwa vya fedha.
Kocha wa United, Ole Gunnar Solskjaer alikwenda kuonana na mchezaji huyo mara mbili na iliripotiwa kuwa anaweza kwenda kwenye kikosi cha United ambacho hakina mshambuliaji wa uhakika zaidi ya Marcus Rashford.
Sasa United watatakiwa kuhakikisha wanafanya kazi ya ziada kumpata mshambuliaji mwingine mwenye kiwango cha juu Ulaya kwa sasa.
Sasa kinda huyo atakuwa akisubiri mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani dhidi ya Augsburg Januari 18.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, inaonekana anaweza kuanza kuwika akiwa hapo baada ya kufanikiwa kufunga mabao nane kwenye michezo sita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Bado anaonekana anaweza kuwika dhidi ya timu kubwa Ulaya kwa kuwa kwenye mabao yake alifanikiwa kuwafunga Liverpool.
Pia aliwafunga wabishi Napoli na Genk jambo ambalo linaonyesha hawezi kusumbuliwa na timu yoyote kigogo barani Ulaya.
Hili ni pigo kwa RB Salzburg, kwa kuwa mchezaji huyo amefanikiwa kufunga mabao 16 na kutoa pasi sita za mabao kwenye timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Austria.
Siyo mchezaji mwenye uzoefu mkubwa sana kwenye soka duniani akiwa amefanikiwa kujiunga na RB mwaka mmoja tu uliopita akitokea Molde ya Denmark. Kwenye maisha yake ya soka amefanikiwa kucheza michezo 93 na kufunga mabao 49.
Munich, Ujerumani