Timu ya Simba SC imejibu mapigo kwa Yanga baada ya leo kumtambulisha kiungo wa kimataifa wa Msumbuji, Luis Jose Miquissone aliyesaini mkataba wa miaka minne akitokea UD Songo.
Simba imemtambulisha kiungo Miquissone leo mchana baada ya watani zao Yanga kumtambulisha kiungo Haruna Niyonzima kutoka AS Kigali jana.
Usajili wa nyota hao wawili unaongeza radha ya mechi ya watani wa jadi itakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa kwa Simba kuikaribisha Yanga.

Kiungo huyo Luis amekabidhiwa jezi na kocha Sven Vandenbroeck tayari kujiunga na kambi ya mabingwa hao wanaojianda na mechi yao ya kesho.
Simba imemsajili Miquissone baada ya kiungo huyo kuonyesha soka la kiwango cha juu pamoja na kufunga wakati timu ya UD Songo ilipoitoa Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu.

Kabla ya kusajiliwa na Simba kiungo huyo wa kimataifa wa Msumbuji alikuwa akihusishwa kutakiwa na Yanga, lakini dakika za mwisho miamba hiyo ya Msimbazi ilifanikiwa kuipata saini yake.