×

Aubameyang: Siondoki Arsenal, Nipo 100%

STRAIKA wa Arsenal, PierreEmerick Aubameyang amewaambia mashabiki wa timu yake kuwa yupo fiti na anajituma asilimia 100 kwa ajili ya timu yake hiyo.

Mara baada ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata dhidi ya Manchester United, Jumatano iliyopita, mchezaji huyo aliwathibitishia mashabiki kuwa akili yake yote ipo Arsenal ambayo kwa sasa ipo chini ya Kocha Mikel Arteta.

Aubameyang amekuwa akihusishwa kuondoka kikosini hapo, hata baada ya ujio wa Arteta ilionekana wazi kuwa hana muda mrefu wa kuendelea kufanya kazi chini ya kocha huyo kijana.

 

Taarifa za kuondoka kwake zimekuwa zikieleza kuwa sababu kubwa ambayo itamuondoa ni kwa kuwa anataka kwenda kwenye timu ambayo atacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 

“Vyombo vya habari va Uingereza vinapenda kuzungumza sana, kwa sasa nipo hapa, ninajituma asilimia 100,” alisema Aubameyang mara baada ya mchezo wa Jumatano.

 

Mbali na hapo, Arteta naye aliweka wazi kuwa hana mpango wa kumruhusu mshambuliaji huyo kuondoka. “Sifikirii kuhusu hilo, hakuna kitu kama hicho,” alisema kocha huyo.

Leave a Comment