
UKIMWAMBIA mtu ataje majina ya wasanii ambao wamewahi kutikisa kwenye Muziki wa Hip Hop duniani ni ngumu kuliacha jina la O’shea Jackson ambaye mashabiki wanamtambua zaidi kama Ice Cube.
Akiwa na umri wa miaka 50 sasa, Ice Cube alizaliwa Los Angeles, California Marekani, akiwa pia na kipaji kikubwa cha uigizaji wa filamu.
Ice Cube, mwenye watoto wanne, ni rapa ambaye alifanya kazi wakati ule wa upinzani mkubwa kati ya wasanii wa East Coast na West Coast, ambao mwishowe ulisababisha mauaji ya mastaa wawili wakubwa, Tupac Shakur na Biggie, ambao wote waliuawa kwa kupigwa risasi.
Akianzia muziki mtaani kama walivyo wanamuziki wengi, Ice Cube alifanya albamu yake ya kwanza iitwayo AmeriKKKa’s Most Wanted mwaka 1990, akiifanya baada ya kuanza muziki na kundi la Hip Hop la C.I.A. na baadaye kujiunga na Niggaz Wit Attitudes (N.W.A) ambako alikuwa pamoja na mkongwe mwingine Dr. Dre na mwaka uliofuata akaanza pia kuigiza filamu akianza na Boyz n the Hood (1991).
Ice Cube anajulikana kama mmoja wa wanamuziki watukutu ambao baadhi ya mashairi ya nyimbo zake yalikuwa ni makali, wakati mwingine yakiwa ya kibaguzi, akiwatukana wazungu na hata kutoa maneno yaliyotafsiriwa kama matusi.
Ice Cube ni mmoja wa wasanii waanzilishi wa Hip Hop ya kiharakati, maarufu kama Gangsta Rap na sehemu kubwa ya muziki wake ni wa kiharakati. Alitajwa kuwepo katika nafasi ya nane na MTV kati ya 10 Bora ya marapa wa nyakati zote (10 Greatest MCs of All Time).

Lakini rapa mwenzake, ambaye naye anatajwa kuwa mtukutu, Snoop Dogg anamuweka Ice Cube kama MC bora kabisa wa miaka yote na mwaka 2012, mtandao wa The Source ulimuweka mwimbaji huyo katika nafasi ya 14 ya waandishi bora 50 wa muda wote.
Baadhi ya albamu zingine zilizofanywa na Ice Cube ni pamoja na Death Certificate (1991), The Predator (1992), Lethal Injection (1993), War & Peace Vol. 1 (The War Disc) (1998), War & Peace Vol. 2 (The Peace Disc) (2000), Laugh Now, Cry Later (2006), Raw Footage (2008) na I Am the West (2010).
Ice Cube amewahi kufanya kolabo na wanamuziki wengine kibao wa Hip Hop kama mwaka 1994 alipoungana na Dr Dre kufanya kibao kilichopewa jina la Natural Born Killaz ambaye pia aliungana naye katika ziara iliyopewa jina la Up In Smoke Tour, mwaka 2000 ikiwajumuisha pia wakongwe wengine kama Eminem na Snoop Dogg.
Katika filamu, baada ya kuwa amefanya vizuri katika filamu yake ya kwanza Boyz n the Hood mwaka 1991, akaingia katika Trespass ambayo alishiriki pamoja na mastaa wengine kama Ice-T na Bill Paxton katika filamu ya mapigano na baadaye akacheza The Glass Shield.
Mwaka 1993 alitakiwa kucheza picha moja la kimapenzi akiwa na staa mwingine mkubwa wa muziki, Janet Jackson iliyoitwa Poetic Justice, lakini akakataa kucheza nafasi aliyopewa, ambayo baadaye ilitolewa kwa Tupac Shakur.
John Singleton alimshawishi Ice Cube kujaribu kuandika simulizi ya filamu, akimweleza kama anaweza kuandika wimbo, basi anaweza kuandika muvi. Baada ya kushawishika, mwaka 1995 akaandika filamu ya vichekesho, ambayo mwenyewe pia alishiriki kucheza akiwa na mchekeshaji chipukizi wakati huo, Chris Tucker.
Filamu hiyo iliitwa Friday iliingiza mapato ya dola milioni 28 dunia nzima.
Amecheza filamu nyingi hadi sasa, lakini pamoja na kuwa hadi sasa bado anafanya muziki, ni wazi kuwa kizazi cha Ice Cube kinaondoka na kuacha historia isiyofutika katika mambo ya muziki, hasa wa kiharakati ambao umezungumza sana kuhusu haki za Wamarekani weusi.
Mwaka 1997 alicheza filamu iliyojizoela umaarufu mkubwa duniani ya Anaconda akiwa na mwanamama Jennifer Lopez ambapo wao ndiyo walikuwa wahusika wakuu na kufanikiwa kuua nyoka mkubwa.
Humo ndani, Ice Cube alionyesha uwezo mkubwa ambao wengi hawakutegema kama ana vipaji viwili, cha muziki na filamu. Tasnia ya burudani hususan kwenye muziki inamkumbuka mkali huyu kutokana na kazi kubwa alizofanya huko nyuma.