×

Kipindi Kinachogusa Hisia za Jamii Chazinduliwa Global TV

Mtangazaji wa kipindi cha Global Jamii, Anna Mbawala na Prodyuza wa kipindi hicho, Anthony Kamonga wakiwasili katika uzinduzi wa kipindi chao uliofanyika leo kwenye ofisi za Global Group, Sinza Mori DSM.

 

TELEVISHENI bora ya mtandaoni, Global TV Online imezindua rasmi Kipindi cha Global Jamii, ambacho ni maalum kwa ajili ya kuwamulika watu mbalimbali wenye mtatizo ya kiafya, kijamii na wenye kuhitaji msaada kutokana na matatizo yanayowazunguka katika jamii wanayoishi.

 

 

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika leo, Jumatatu katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam ikiongozwa na Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally ‘Jembe’ na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo, Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho, wafanyakazi.

 

Wafanyakazi wa Global wakifurahia kwa kucheza ngoma wakati Anna na Kamonga walipowasili.

 

Pia hafla hiyo imehudhuriwa na mgeni mwalikwa, Mohammed Bane ambaye aliwahi kufanyiwa mahojiano na Global Jamii baada ya kunusurika kifo kufuatia kugongwa na treni wakati akitoka shule na mikono yote miwili na mguu mmoja kukatika.

Mkurugenzi wa Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo akizungumza wakati wa hafla hiyo.

 

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Shigongo amesema: “Nawapongeza sana timu yote ya Global Jamii na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri wanayoifanya.

 

“Nafahamu ugumu wa kufanya kazi hii kwa sababu hata mimi niliwahi kufanya miaka 20 iliyopita wakati naanzisha kampuni Global Publishers, nilikuwa nikienda hadi vijijini kuhoji watu mbalimbali wenye matatizo makubwa, hivyo napenda kuwatia moyo endeleeni kuongeza bidii.

 

Wafanyakazi wa Global Group wakifuatilia kwa makini hafla ya uzinduzi huo.

 

“Kusema kweli kipindi hiki kinagusa maisha ya watu moja kwa moja na kinawasaidia watu wengi kupitia nyinyi. Wapo waliokuwa hawana fedha za matibabu lakini kupitia kipindi cha Global Jamii wameweza kuonwa na wasamaria wema, mashirika na taasisi mbalimbali.

Wakitazama baadhi ya vipindi vilivyowahi kufanywa na Global Jamii.

 

“Wapo ambao wamewasaidiwa kupelekwa hata India kwa ajili ya matibabu, na kunusuru maisha yao, kwa hiyo msichoke kazi hii ni kama utume, endeleeni kuisaidia jamii, sisi tutaendelea kuwasapoti kwa nguvu zote,” alisema Shigongo.

Mhariri Mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally ‘Jembe’ akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

 

Aidha, Shigongo alitumia nafasi hiyo kumtia moyo kijana Mohammed ambaye kwa sasa yupo kidato cha nne na kumtaka kutokata tamaa kwani ipo sababu kubwa ya Mungu kumbakisha mzima baada ya ajali ya kugongwa na treni, huku akimuahidi kuwa Kampuni ya Global Group itagharamia masomo yake ya kidato cha tano na sita.

 

Kamonga akitoa neno la shukrani.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Global Group, Abdallah Mrisho amewapongeza waandaaji wa kipindi hicho na kuwataka wafanyakazi wengine wa Global TV Online kuendelea kuwapa ushirikiano na kuongeza ubunifu zaidi katika vipindi vingine vinavyorushwa kwenye televisheni hiyo.

 

Anna Mbawala akitoa neno la shukrani.

 

Naye Mhariri Mtendaji, Saleh Ally amesema; “Napenda kuwaambia nyinyi mnaoendesha kipindi hiki, Anna na Kamonga, uzinduzi wa kipindi hiki uwe chachu ya kufanya kazi bora zaidi, sisi tunaamini ninyi ni bora na mnaweza kukifanya kipindi hiki kiikuze Global na kuwakuza na nyinyi wenyewe.

 

Kijana Mohammed Bane akikabidhiwa vifaa vya shule.

 

“Desturi ya Global miaka yote ni kufanya kazi kwa ukaribu na jamii inayotuzunguka, tumejitoa kuisaidia jamii na kupitia kipindi cha Global Jamii, tunaamini watu wengi watatatuliwa matatizo yao na kupata misaada ili waweze kuzifikia ndoto zao, “ alisema Saleh.

Shigongo akimpa neno la faraja Mohammed.

 

Kwa upande waendeshaji wa kipindi hicho, Anna na Kamonga kwa pamoja walitoa shukrani kwa uongozi na wafanyakazi wote wa Global Group, kwa ushirikiano wanaowapa katika kufanikisha kazi yao, huku wakiahidi kujituma zaidi licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakiwa wanafanya kipindi hicho.

 

 

Sambamba na hilo timu ya Global Jamii, ilitoa vifaa mbalimbali vya shule vikiwemo madaftari, viatu, sare za shule, tranka, traki suti na vifaa vingine ambavyo vitamsaidia katika masomo yake.

 

Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdallah Mrisho akitoa hamasa na pongezi kwa vijana hao pamoja na wafanyajkazi wa Global Group.

 

Kipindi cha Global Jamii huruka kupitia  GLOBAL TV ONLINE

 

Picha ya pamoja ya baadhi ya wafanyakazi wa Global group na kijana Mohammed.

 

 

HABARI/PICHA: RICHARD BUKOS/ GPL  

   

Leave a Comment