×

Magoti, Mwenzake Wazidi Kusota Rumande

UPANDE wa Jamhuri umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika kesi inayimkabili Ofisa Elimu kwa Umma wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti (26) na mwenzake, Theodory Gyan (36), kuwa upelelezi katika shauri hilo upo katika hatua nzuri kukamilika.

 

Hayo ameyaeleza wakili wa serikali, Renatus Mkude, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwamo la utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh. Milioni 10 ambapo ameomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

 

Upande wa utetezi akiwemo Wakili Anna Henga ambaye ni Mkurugenzi wa LHRC, umeomba upande wa jamhuri kuharakisha upelelezi huo ili shauri hilo liweze kusikilizwa kwa wakati.

 

Akijibu hoja hiyo,  wakili wa serikali amesema watajitahidi kuharakisha upelelezi huo kwani mbali na kuhusisha jeshi la polisi pia unahusisha vyombo vingine.

 

Magoti na mwenzake walifikishwa mahakamani hapo Desemba 24, 2019,  na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon,  akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi na Faraja Nchimbi.

 

Washtakiwa hao wawili wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019,  ndani ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania kwa pamoja na watu ambao hawapo mahakamani,  kwa makusudi walishiriki makosa ya kiuhalifu ya kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kufanya kosa la jinai na kuwawezesha kujipatia kiasi cha Sh. Mil 17,354,535.

 

Katika shtaka la pili,  inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, 2019,  ndani ya jiji na mkoa wa Dar es Salaam, kwa pamoja washtakiwa hao na wengine ambao hawapo mahakamani, walimiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kutenda makosa.

 

Katika shtaka la tatu, inadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi, 2019 na Desemba 17, mwaka huu, ndani ya jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walijipatia jumla ya Sh. 17,353,535 wakati wakijua mapato hayo yametokana na kushiriki genge la uhalifu.

 

Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 21, 2020, itakapotajwa. Washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana kesi ya uhujumu uchumi kutokuwa na dhamana.

 

NDUGU WA TITO MAGOTI WALIVYOFURIKA MAHAKAMA YA KISUTU

Leave a Comment