
BABA mzazi wa mtoto anayedaiwa kubakwa (jina linahifadhiwa); Mbwana Said (42), ameeleza kusudio la kumfunga jela baba yake mzazi, Said Mbwana (68) kwa tuhuma za ubakaji wa mjukuu wake. Kwa mujibu wa baba wa mtoto huyo wa kike mwenye umri wa miaka 11, takriban miezi minne iliyopita baba yake huyo ambaye ni Mjumbe wa Shina Namba 9 -Mtaa wa Miraji Tegeta B jijini Dar, alitokomea kusikojulikana baada ya tuhuma hizo nzito.
Baba huyo alieleza kuwa, tukio hilo lilijiri oktoba 26, mwaka jana ambapo babu huyo alidaiwa kufanya kitendo hicho kwa mara ya pili ndipo majirani walipovalia njuga suala hilo kwa kuripoti Polisi. Alisema siku ya tukio, bibi wa mtoto huyo alitoka kwenda kwenye kazi zake ndipo babu yake akatumia mwanya huo kufanya kitendo hicho.
“Siku hiyo mama yangu (bibi wa mtoto aliyebakwa) alitoka kwenda kwenye shughuli zake maana huwa ni kungwi, kwa hiyo alikwenda kufunda mwali ndipo baba yangu akaingia kwenye chumba ambacho wanalala wajukuu.
“Walikuwa wamelala watoto watatu, wengine ni wa ndugu zangu na katika chumba kile mlango huwa unafungwa na msumari kwa ndani. Kwa kuwa wote huwa tunaaminiana na sikujua kama baba angeingia mule ndani.
“Baada ya kuingia chumbani humo alikuta watoto wamelala na nakumbuka ulikuwa muda wa saa saba usiku hivi. “Alipoingia chumbani humo alimchukua mwanangu kisha alikwenda naye chumbani kwake na kumfunika kwa kitambaa usoni.
“Baada ya hapo ndipo akamfanyia unyama huo huku akimuonya kutokusema na kama akisema atamuua,” alieleza baba huyo. Baba huyo aliendelea kusema kwa uchungu kuwa, wakati akifanyiwa kitendo hicho, alihisi maumivu makali hivyo akawa anapiga kelele.
Alisema baada ya kuona hivyo, mtuhumiwa huyo alitoka nduki na watu walipokwenda kumtazama mtoto huyo walimkuta akilia kutokana na maumivu aliyoyapata.
“Tulimkuta analia, akaniambia babu kamfanya kama alivyomfanya siku ile (alipombaka mara ya kwanza), yaani ni kwamba alishawahi kumbaka mara ya kwanza, kwa kuwa tuliona ni jambo la fedheha, tukamaliza kifamilia na kumkanya.
“Kwa tukio hili la pili ndipo ikabidi nimchukue mtoto na kwenda naye Kituo cha Polisi cha Madale (Tegeta) na nikampeleka Hospitali ya Sinza, Palestina, akapimwa kisha tukarudi kituo cha Polisi.
“Pale kituo cha Polisi niliambiwa nimtafute mtuhumiwa, akipatikana niwajulishe, lakini bado hatujampata,” alisema.
Alisema majirani zake wamemwambia kuwa endapo baba yake atarudi na kupokelewa watamshtaki yeye pamoja na baba yake.
“Hili la mara ya pili ni gumu kwa sababu mara ya kwanza baada ya kufanya tukio aliondoka, baada ya miezi mitatu akarudi na tukayamaliza kifamilia,” alisema baba huyo na kuongeza; “Kiukweli safari hii lazima nimfunge baba yangu.”
Kwa upande wake, bibi wa mtoto huyo, Amina Salumu ambaye ni mke wa mtuhumiwa huyo alisema amechoshwa na tabia za mumewe na kwamba siyo mara yake ya kwanza na amekuwa akiwafanyia watoto wa watu wengine.
“Mume wangu amekuwa na tabia hizi tangu tukiwa vijana tulipokuwa kwenye nyumba za kupanga hadi sasa tumejenga nyumba yetu.
“Nimekuwa ninamkanya sana kwa muda mrefu, lakini naambulia kipigo kiasi kwamba alishaniumiza jicho na bega, kwa hiyo ninaiomba Serikali inisaidie, aweze kupatikana,” alisema bibi huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Mussa Taibu alisema taarifa za tukio hilo hazijafika mezani kwake. “Sijapata taarifa kuhusu tukio hilo, kwa hiyo nitalifuatilia,” alisema Kamanda Taibu