
PAULA ni mtoto wa staa wa filamu Bongo; Kajala Masanja na Prodyuza maarufu hapa nchini Paul Matthyes ‘ P.Funky. Jina lake limekuwa masikioni kwa watu mbalimbali kutokana na umaarufu mkubwa walionao wazazi wake japokuwa wazazi wake hao hawaishi pamoja kutokana na changamoto mbalimbali za maisha.
Paula ambaye wiki iliyopita yeye na mama yake walikula shavu la kutangaza taulo za kike aina ya Rania ambayo yeye mwenyewe anasema kuwa nguvu kubwa mpaka anapata shavu hilo anamshukuru sana mama yake kwani bila yeye asingefika hapo alipo.
Mwandishi wetu amefanya mahojiano maalumu na Paula ambapo msichana huyo amezungumza mengi yanayozunguka maisha yake.
Risasi Jumatano: Hongera Paula, ilikuwaje mpaka ukapata na wewe dili hilo na siyo mama yako pekee?
Paula: Nadhani ni Mungu aliamua kutubariki mimi na mama yangu.
Lakini kikubwa napenda kumshukuru mama, pia inawezekana bila yeye nisingepata ubalozi huu.
Risasi Jumatano: Kwa nini unasema bila yeye usingepata?
Paula: Kwa sababu walimuangalia na mama yangu jinsi anavyoniweka kama mtoto wa kike, kila unachoniona ni mama yangu ananite-ngeneza.
Risasi Jumatano: Kwa hiyo mama yako ndiyo anafanya kila kitu kwenye maisha yako na sio baba?
Paula: Baba ni baba siku zote na ataendelea kuwa baba yangu, lakini mama yangu ndiyo jasiri wa maisha yangu; ninapolia tunalia wote, nipopata shida mimi yeye ndiyo wa kwanza kuumia na atajitahidi niwe sawa.
Risasi Jumatano: Watoto wengi wa kike wanapolelewa na mama pekee wanakuwa wanajisahau na kuona mama kama ni dhaifu na kufanya mambo mengi ambayo sio mazuri, vipi kwa upande wako?
Paula: Labda niseme leo, mama yangu ni mama rafiki sana katika dunia hii, lakini ni mama mkali mno ambaye bado sijapata kuona mwingine, hivyo hapendi mchezo na mimi nafahamu hilo.
Risasi Jumatano: Kwa hiyo baba na mama nani mkali?
Paula: Uzuri niliwahi kuishi na baba pia, lakini mama ni mkali sana na ukali wa mama umenifundisha mengi sana labda nisingekuwa hivi.
Risasi Jumatano: Wewe unafurahia ukali wa mama yako?
Paula: Ndiyo nafurahia kwa sababu unanifanya niwe binti mzuri, unajua mama amepitia mengi katika maisha yake hivyo hataki na mimi nipite huko.
Risasi Jumatano: Ushawahi kukutana na vishawishi vya hapa na pale kutoka kwa wanaume?
Paula: Nilimsogeza mama yangu kuwa rafiki yangu mkubwa sana kwenye hii dunia, jaribu lolote linalotaka kunikumba namshirikisha yeye na ananipa mbinu nzuri tu hivyo nawakwepa sana hao watu.
Risasi Jumatano: Hivi sasa unaingia kidato cha ngapi?
Paula: Naingia kidato cha sita.
Risasi Jumatano: Kutokana na maneno mengi baada ya kutofanya vizuri mtihani wako wa kidato cha nne, unawaahidi nini watu ambao walikuchukulia tofauti?
Paula: Wajue tu ukianguka mara moja siyo siku zote, wategemee mambo mazuri kwenye matokeo ya kidato cha sita.
Risasi Jumatano: Asante, kwa ushirikiano wako.
Paula: Asante sana.
Makala: Imelda Mtema