
NDOA usiichukulie poa ina sarakasi nyingi; kama hii ya mke na mume kufikishana Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Temeke huku tendo la ndoa likitajwa kuwagombanisha. Maulidi Hatibu (38) na mkewe, Shani Kitwana (33), wakazi wa Temeke jijini Dar walizua tafrani Bakwata ambapo mke alimwambia Shehe wa baraza hilo, Omary Rubaha kuwa hana anachokitaka kwa mumewe zaidi ya talaka kwa vile mwandani wake amekuwa akimuita malaya.
Aliongeza kuwa, mbali na kuitwa hivyo mumewe amekuwa akimpiga mara kwa mara kwa kumtuhumu ‘kuchepuka’ nje ya ndoa.
“Kingine kinachoniuma ni kwamba huyu mwanaume alishawahi kutaka kushiriki tendo la ndoa na mimi wakati nikiwa na siku moja baada ya kujifungua,” alisema Shani. Mwanamke huyo aliendelea kudai kuwa mara kadhaa mumewe amekuwa akiwashutumu ndugu zake kuwa ndiyo wanaomchochea aombe talaka jambo ambalo alisema si kweli bali kinachomsukuma kutaka kutengana naye ni tabia zake mbaya.
“Nimechoka na mateso na vipigo nakumbuka mume wangu alinifukuza nikiwa na mimba ya miezi tisa na kuniambia kuwa mimi nina gundu nikikaa naye hapati riziki. “Nilipojifungua akaja na madai mengine kuwa mtoto siyo wake hivyo nikaamua twende kupima DNA, tulipofika hospitali alikataa kupima,” alisema Shani.
Wakati mwanamke huyo akimtuhumu hivyo mumewe mbele ya shehe, kwa upande wake Maulidi alijitetea kuwa ndoa yao ina mwaka na nusu, lakini mkewe amekuwa na tabia ya kutomsikiliza na kusikiliza zaidi ndugu zake.
“Kuna siku mvua ilikuwa inanyesha akapigiwa simu na mwanaume (akimaanisha mchepuko wa mkewe) akawa anaongea naye kimahaba huku akimwambia kuwa yuko tayari kutoka naye.
“Nilikasirika sana kwa jambo hilo alilolifanya mbele yangu lakini kwa kuwa napenda amani nilimsamehe mke wangu,” alisema Maulidi na kutupilia mbali tuhuma kuwa alitaka kutembea na mkewe akiwa ana siku moja baada ya kujifungua.
Hata hivyo, Shehe Omary ambaye ni mmoja kati ya viongozi wa baraza Kitengo cha Usuluhishaji Kesi za Ndoa alikiri kupokea malalamiko hayo na kubainisha kuwa hayupo tayari kuandika hati ya talaka kwa kuwa baraza lipo kwa ajili ya kuwaunganisha watu na siyo kuwatenganisha.
Waandishi: Memorise Richard na Khadija Bakari