×

Lala Salama ya Usajili wa Laini, Macho yote kwa JPM

“JPM (RAIS Dk John Pombe Magufuli), okoa jahazi, laini zetu zipone!” Hayo ni maneno ya baadhi ya wamiliki wa laini za simu zaidi ya shilingi milioni 22 ambazo zinatarajiwa kukatiwa mawasiliano leo kwa kuwa hazijasajiliwa kwa alamu za vidole.

 

Kilio hicho kinatokana na muda wa siku 20 ambao uliongezwa na Rais Magufuli ili kuwezesha zaidi ya Watanzania milioni 10 ambao hawajasajili laini zao kutokana na kukosa namba za vitambulisho vya Taifa, waweze kusajili.

 

Hata hivyo, muda huo wa nyongeza haukutosha na sasa macho na masikio yote yameelekezwa tena kwa Rais Magufuli kwa mara nyingine ili atoe tamko litakalookoa laini milioni 22 kati ya milioni 48 ambazo zitafungwa kuanzia leo saa sita usiku.

 

Awali, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuwa Desemba 31, mwaka jana, ingekuwa siku ya mwisho ya kutumika laini zisizosajiliwa kwa mfumo huo, lakini Rais Magufuli aliongeza muda hadi Januari 20, mwaka huu.

 

Rais Magufuli alisema anaongeza muda huo ili watu walioshindwa kusajili namba zao kwa sababu ya kuugua na wasiokuwa na namba au Vitambulisho vya Taifa, waweze kumalizia mchakato huo.

 

Licha ya kwamba alisema muda huo ukiisha, hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na kuiagiza TCRA kuzima laini zisizosajiliwa, hali sasa imeonekana kuwa tete kutokana na takwimu zilizotolewa Januari 12, mwaka huu kudhihirisha kuwa bado kundi kubwa la watu limekwama kutokana na kutopata namba za Vitambulisho vya Taifa.

 

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakiyanjala, alisema hadi kufikia Januari 12, mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

 

“Laini za simu 22,478,727 sawa na asilimia 46.3 bado hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole,” alisema Mwakiyanjala.

Takwimu zinaonesha hadi Desemba 10, mwaka jana, laini zilizokuwa zinatumika zilikuwa 47,063,603 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1.

 

UCHACHE WALIOPATA VITAMBULISHO, NAMBA

Itakumbukwa kuwa Aprili, mwaka jana, Rais Magufuli alisema Watanzania milioni 14 ndiyo waliokuwa wamepata Vitambulisho vya Taifa.

Aidha, takwimu zilizotolewa Januari 2, mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk Anold Kihaule, zinaonesha watu milioni 7.6 tayari wana namba na kila siku mamlaka hiyo inaendelea kuzitoa sehemu mbalimbali nchini.

 

Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa bado kundi kubwa la watu hawajapata namba na Vitambulisho vya Taifa, hivyo kukwamishwa kusajili laini zao na kuelekeza lawama zao kwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

 

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Gazeti la IJUMAA Wikienda, walisema NIDA imekuwa kikwazo kwa kupata namba na vitambulisho kwa wakati kutokana na uzembe unaosababishwa na baadhi ya maofisa wanaoandikisha raia.

 

Lakini pia baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa, kupungua kwa kasi ya uandikishaji katika kipindi cha awali, ambayo ilitokana na mkwamo wa kibajeti ndani ya mamlaka hiyo, ndiyo chanzo cha watu wengi kuchelea kujiandikisha mapema.

 

Haruna Hussein, mkazi wa Morogoro alisema; “Nimefuatilia namba yangu ya NIDA tangu mwezi wa sita mpaka sasa sijapata namba yangu, tunapata taabu kwa sababu pia ya umbali wa ofisi za NIDA.”

 

Naye Emannuel Kisima, Mkazi wa Ilala, alisema kwa upande wake licha ya kujiandikisha kupata kitambulisho tangu Novemba, mwaka jana, alikuja kubaini majina yake yamekosewa baada ya kuuliza kupata namba ya kitambulisho.

 

“Kwa hiyo imebidi niende Mnazi-Mmoja kufanya marekebisho na tumeambiwa majibu ni baada ya wiki mbili, kwa hiyo hili ni jambo ambalo limetukwamisha wengi wetu kukosa namba za vitambulisho,” alisema.

 

Hata hivyo, Novemba, mwaka jana, Rais Magufuli alilazimika kumuita Mkurugenzi wa NIDA, Dk Kihaule baada ya kupokea malalamiko ya wananchi wa Mji wa Morogoro ambao walilazimika kutoka wilaya kufuata vitambulisho katika ofisi za mikoa.

 

“Tunamuomba Rais aingilie kati suala hili kwa sababu wengine tunakosa nauli za kuja katika ofisi za mikoa, ingetakiwa NIDA wajipange ili wafungue ofisi katika vijiji na kata zote nchini badala ya kuelekea wilayani au mkoani ili kupunguza misururu ya watu wanaohitaji vitambulisho hivyo,” alisema mkazi wa Goba.

 

Naye Richard Bukos wa Dar alisema, alijiandikisha mwaka 2016, lakini hadi leo hajapata kitambulisho na akienda NIDA anaambiwa mfumo wa picha ulikosewa, hivyo aanze upya usajili.

 

TCRA: ZOEZI KUWA ENDELEVU

Wakati hayo yakijiri, TCRA imesema zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni endelevu, hivyo kwa watakaositishiwa huduma za laini za simu, wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la kuzirudisha au kupata laini mpya.

 

“Kwa watumiaji au waombaji wapya wa laini za simu, wataendelea kusajiliwa muda wote na usajili huo kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole ni endelevu,” alisema Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Mwakiyanjala.

TCRA pia ilisema kwa wanadiplomasia au taasisi ambazo hazijakamilisha usajili wa laini za simu au zinazotumika kwenye vifaa vyao vya mawasiliano, wanatakiwa waendelee kufuata utaratibu uliowekwa.

STORI: GABRIEL MUSHI, DAR

Leave a Comment