
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu (26), amejiunga tena na Klabu yake ya zamani ya TP MAZEMBE ya nchini DR Congo.
TP Mazembe kupitia page yake ya Instagram imetangaza kurejea kwa mchezaji huyo ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia waajiri wake hao wa zamani. Wakati huo TP Mazembe imeachana na kiungo wake Nathan Sinkala raia wa Zambia.
Ulimwengu aliondoka Mazembe mwaka 2016 akiwa na ndoto ya kwenda kucheza soka Ulaya lakini kwa bahati mbaya haikuwa kama watu wengi walivyotamani baada ya nyota huyo kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara.
Mwaka 2017 na 2018 alijaribu bahati yake katika vilabu viwili vya Ulaya, Eskilstuna (Sweden) na FC Sloboda Gorazde (Bosnia) huku akiwa na imani huenda ikiwa mwanzo wa safari yake ya kupata vilabu vingine vikubwa vya Ulaya.
Baadaye Tom alirejea tena Afrika na kujiunga na Al Hilal ya Sudan lakini hakudumu kwa muda mrefu akajiunga na JS Soura ya Algeria. Jumatano hii Ulimwengu atatambulishwa rasmi na klabu yake ya zamani huko Lubumbashi-Congo DR.