KISA hiki cha mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Anna Nguvila (22), mkazi wa Kitongoji cha Isoko Kijiji cha Igundu Kata ya Sangambi Wilaya ya Chunya jijini hapa kinasikitisha mno.
Anna anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa mahojiano zaidi kufuatia tukio la kumzika porini mwanaye wa kiume, Junior Anjelo (2), baada ya kufariki dunia akiwa njiani kumpeleka hospitalini.
Tukio la Anna kumzika mwanaye lilibainika hivi karibuni baada ya mwanamke huyo kurejea kijijini hapo bila mtoto tangu alipoondoka kwenda Kijiji cha Mapogolo kuuza pombe ya kienyeji kisha akarudi bila mtoto.
Mtendaji wa Kijiji cha Igundu, Joseph Nangale alisema Anna alisema, alimzika mwanaye huyo baada ya kufariki dunia akiwa njiani kumpeleka hospitalini katika Kijiji cha Isoko akitokea Mapogolo.
Baada ya mahojiano, Anna alikiri kumzika mwanaye huyo porini.
Baada ya mahojiano kwenye ofisi ya kijiji, Nangale alitoa taarifa Polisi ambapo walikwenda eneo alilomzika mtoto na kulazimika kufukua mwili wa mtoto kisha kuuhifadhi chumba cha maiti kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
Theresia Mwendapole ni Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Chunya ambaye alisema kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo si cha kiungwana kwani kama mtoto alifariki dunia alipaswa kutoa taarifa kijijini badala ya kuamua kumzika peke yake.
“Kila binadamu anastahili heshima hivyo kitendo cha mwanamke huyo kumzika mwanaye peke yake kina walakini,” alisema Theresia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi (PICHANI) alisema kuwa, kitendo hicho ni cha kinyama kwani kama mtoto alifariki dunia, mama huyo alipaswa kutoa taarifa kwa wananchi ili asaidiwe kumzika, jambo ambalo Anna hakulifanya.
Mahundi alisema, asasi mbalimbali zinapinga ukatili dhidi ya watoto na wanawake, lakini vitendo hivyo vinapofanywa na mwanamke haipendezi.
Alisema kuwa, Jeshi la Polisi likikamilisha uchunguzi wake, mtuhumiwa huyo afikishwe mahakamani ili kubaini ukweli wa tukio hilo lililoacha simanzi kubwa kijijni hapo.
Stori: Ezekiel Kamanga, Mbeya
