Kiongozi wa Kanisa la International God’s Way la Ghana, Askofu Daniel Obinim ametangazia wafuasi wake kuwa anauza mafuta yanayoweza kuwakinga na Coronavirus.
Obinim ambaye mtindo wake wa maisha ya anasa ni gumzo Ghana, anauza chupa moja ya mafuta hayo kwa Cedi 200 za Ghana (TZS 85,000).
Askofu huyo alizindua mafuta hayo jana Jumapili wakati wa ibada ambapo alisema alifanya hivyo ili kuhakikisha ugonjwa huo haufiki katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Mwaka jana Obinim alizua wimbi kubwa katika vyombo vya habari alipowaambia wanawake katika moja ya ibada zake kwamba ana uwezo wa kuongeza ukubwa wa makalio yao bila ya kutumia upasuaji (plastic surgery).
Anadai kuwa ugonjwa huo wa corona uliozuka Desemba mwaka jana nchini China, ulikuwa ukimnyima usingizi kwa kuhofia ungefika nchi za magharibi mwa Afrika ndipo malaika wa Mungu alipomtokea na kumpa mafuta hayo.
Ameongeza kuwa mafuta hayo yameshathibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa ya mbinguni ‘Heaven’s Division of Food and Drugs Authority’ hivyo hayahitaji kuthibitishwa tena na mamalaka za Duniani.
Miaka ya nyuma askofu huyo aliwahi kutangaza kuwa ananamba za simu za Mungu, ambazo huzitumia kuwasiliana nae.
