VYOMBO mbalimbali vya habari nchini Marekani vimethibitisha kuwa mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu, Kobe Byrant (41) na mwanaye, Gianna Maria-Onore Bryant ‘Gigi’ (13), wamezikwa kwa siri Februari 7, 2020, katika makaburi ya Pacific View Memorial Park, eneo la Corona del Mar mjini California (kulingana na cheti cha vifo) ikiwa ni wiki mbili tangu vifo vyao vitokee.
Kobe, Gigi na watu wengine saba walipoteza maisha katika ajali ya helikopta iliyotokea Januari 26 katika eneo la Calabasas, California. Walikuwa wakielekea kwenye mchezo wa kikapu.
Inaelezwa kuwa maziko hayo awali yalipangwa kufanyika katika makaburi ya Westwood Village Memorial Park kabla ya kubadilishwa, ambapo yalihudhuriwa na wanafamilia pekee na watu wachache wa familia ya Kobe.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mke wa Kobe, Vanessa Bryant, amethibitisha kuwa maombolezo ya pamoja ya vifo vya mumewe na mtoto wake yatafanyika Februari 24 katika Uwanja wa Staples Center.




