×

Mwalimu Mkuu Mbaroni Kwa Ulawiti Mwanafunzi

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Chekechea ya Future iliyopo Msongola, Ilala jijini Dar, yamemkuta mazito. Mwalimu huyo aliyetajwa kwa jina moja la Pidi, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za ulawiti wa mwanafunzi wake wa kike mwenye umri wa miaka mitano. Mwalimu Pidi anadaiwa kumfanyia mwanafunzi huyo ukatili huo, Februari 3, mwaka huu ndani ya eneo la shule hiyo.

Baada ya kupata habari hizo, wanahabari wetu walifunga safari hadi nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo ili kujua mkasa kamili. Akizungumza na wanahabari wetu, mama mzazi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Salma Ramadhani, alikuwa na haya ya kusema;

“Mwanangu anasoma chekechea hapo kwenye hiyo shule inayoitwa Future. “Kawaida huwa wanakwenda saa mbili asubuhi na kurudi saa kumi na moja jioni. “Februari 3, mwaka huu, mwanangu alipokwenda shuleni alikaa hadi muda huo bila kurejea nyumbani. “Ilipofika saa kumi na mbili kasoro jioni, nikiwa nataka kwenda kumuulizia, ghafla nilimuona anarudi.

“Mwanangu alirudi akiwa mnyonge sana tofauti na siku nyingine ingawa sikuwa makini kumchunguza kutokana na ubize wa majukumu ya nyumbani. “Ilipofika usiku kabla ya kwenda kulala, aliniambia mama huku (sehemu za siri) kunaniuma… “Aliniambia huku akinionesha sehemu zake makalioni. “Kwa kuwa kuna kazi nilikuwa nafanya, nikamwambia nitakutazama vizuri mwanangu nisubiri kidogo. “Baada ya muda, mwanangu alilala na baba yake (Abdul Digira) naye alirudi.

“Nilimuhadithia baba yake kuanzia mwanaye alivyochelewa kurudi na aliporudi na kuniambia anajisikia maumivu sehemu za makalioni. “Alipomaliza kunisikiliza, aliniwashia tochi ya simu na kuniambia nimkague kwa maana yule ni mtoto wa kike. “Nilipomkagua, nilipigwa na butwaa baada ya kuona akitokwa na haja kubwa. “Nilipomkagua vizuri, nilizidi kushangaa baada ya kukuta njia yake ya haja kubwa ikiwa imetanuka tofauti na kawaida maana siku zote mimi ndiye ninayemuogesha.

“Nilimueleza baba yake ambaye alinishauri twende Polisi usiku huohuo. “Tulikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Msongola ambapo walitupa PF-3 (hati ya matibabu) na kutuambia kwanza tumpeleke mtoto hospitalini akafanyiwe uchunguzi na kupata matibabu kisha turudi kituoni hapo.

“Tulimpeleka hospitalini ambapo daktari aliyemfanyia uchunguzi alithibitisha mwanangu alipenyezwa na kitu fulani sehemu ya njia ya haja kubwa. “Tulimuuliza mwanangu mara kadhaa kilichomkuta ambapo mara zote alikuwa akirudia kutuambia kuwa Mwalimu Mkuu alimwambia anampaka dawa huku (akionesha makalioni kwake).

“Baada ya uchunguzi wa daktari, tulirudisha majibu Polisi na kufungua jalada la kesi ya kulawiti yenye namba MSL/RB/117/2020 – ULAWITI.

“Baada ya kuripoti tukio hilo, mwalimu huyo alisakwa na kukamatwa ambapo kwa sasa anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Chanika jijini Dar. Wanahabari wetu walifika kwenye shule hiyo muda wa mchana na kukuta hakuna mwanafunzi hata mmoja, ambapo majirani walisema baadhi ya wazazi waliwahamisha watoto wao kufuatia sakata hilo.

Wanahabari wetu walizungumza na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP), Zuberi Chembera ambaye alisema bado taarifa ya tukio hilo halijamfikia mezani kwake na kuahidi kulifuatilia ili sheria ichukuwe mkondo wake.

 

HABARI; NEEMA ADRIAN NA RICHARD BUKOS, UWAZI

Leave a Comment