IDADI ya waliofariki kwa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona imefikia 1,113, huku watu 38,800 wakiendelea na matibabu na maafisa wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wakitangaza kuwa kiwango cha maambukizi mapya bado hakijapungua.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa China nchini, hadi Februari 11, mwaka huu, China kulikuwa na watu 44,653 waliothibitika kuugua ugonjwa huo na kati yao 4,740 walipona na kuruhusiwa.
Hadi Februari 11, mwaka huu, watu 16,067 walikuwa wanasubiri majibu ya vipimo. Pia kufikia Februari 11 raia wa kigeni 27 kwa pamoja nchini China walithibitishwa kuambukizwa virusi vipya vya corona na hakuna Mtanzania.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa kati ya kesi 27 zilizothibitishwa, saba wamepona na wameruhusiwa kutoka hospitalini, wawili wamekufa akiwamo raia wa Marekani, mmoja ni raia wa Japan na 18 wanapata matibabu katika eneo maalumu.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa nje ya Hubei idadi ilipungua na kufikia 377 ikiwa ni siku ya nane mfululizo, huku idadi mpya katika mji ikipungua na kufikia chini ya 2,000 kwa mara ya kwanza.
Kadhalika taarifa hiyo, ilieleza kuwa kuna ongezeko la viwango vya uponaji nchini kote katika mji wa Wuhan, Hubei na China kwa ujumla kwa kuwa vilipanda hadi kufikia asilimia 6.2, 6.1 na 8.2 ikilinganishwa na asilimia 2.6, 1.7 na 1.3 mnamo Januari 27.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Dk. Tedros Ghebreyesus, alikaririwa akisema asilimia 99 ya kesi za ugonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) ziko China na asilimia 97 ya vifo ni katika Jimbo la Hubei.
Katika mkutano wa 146 wa Bodi Kuu ya Wakurugenzi ya WHO alipongeza mkakati wa China katika kupambana na ugonjwa huo. Kwa mujibu wa Dk. Ghebryesus, mkakati wa China ni kuchukua hatua kali katika eneo kuu, chanzo, ili kulinda watu wa China na kuzuia kuenea kwa virusi hivyo katika nchi nyingine.
“Kama isingekuwa juhudi za China, idadi ya kesi zilizo nje ya China zingekuwa kubwa zaidi,” alisisitiza Dk. Tedros.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa, timu ya awali ya wataalamu wa kimataifa inayoongozwa na WHO imewasili nchini China na kwamba watabadilishana kwa kina na wenzao wa China kuhusu hali hiyo na pia kuzuia na kudhibiti janga.
BALOZI WA TANZANIA
Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, anawasiliana kwa karibuni na wanafunzi wa Tanzania walioko Wuhan. “Tunarudia ushauri wa Balozi kwamba njia salama kabisa iliyopendekezwa na WHO ni kukaa Wuhan, epuka kukusanyika na fuata kanuni za usafi. Mamlaka na vyuo vikuu huko Wuhan vitaendelea kuwajali na kutoa msaada kwa wanafunzi wa Tanzania na wa nchi nyingine,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali ya Jimbo la Hubei imechukua hatua kadhaa za kuwalinda wanafunzi wa kigeni dhidi ya maambukizo ya virusi na kukidhi mahitaji yao ya kila siku na mwongozo wa kisaikolojia, pamoja na kuanzisha timu maalumu kutunza wanafunzi wa kigeni, utoaji wa milo ya bure kila siku, na barakoa (masks).
Vile vile, dawa za kuua wadudu, wamepanga wafanyakazi wa China kununua nakala za matumizi ya kila siku kulingana na ombi la wanafunzi wa kigeni na ufunguzi wa simu za moja kwa moja ili kutoa msaada katika maisha ya kila siku na ushauri wa kisaikolojia.
Ubalozi huo ulisema kuwa licha ya ugonjwa huo, uchumi wa China ni imara na ina nguvu, rasilimali na uwezo wa kukabiliana na dharura.
Benki ilitengeneza mpangilio maalumu wa sera kwa kutoa mikopo ya upendeleo ya jumla ya RMB bilioni 300 (Dola za Marekani bilioni 43) kwa wafanyabiashara muhimu wanaohusika katika uzalishaji, usafirishaji au uuzaji wa vifaa muhimu vya matibabu na mahitaji ya kila siku.
“Tuna hakika kwamba China haitashinda tu vita ya kupambana na janga, lakini itapunguza athari za janga kwenye uchumi wake,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
