Uongozi wa Mbao FC umethibitisha kusitisha mkataba wa kocha wake Hemed Morocco na msaidizi wake Abdulmutik Hajji baada ya makubaliano ya pande zote mbili, kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo kwenye ligi kuu Tanzania Bara.
Hadi sasa Mbao FC ina pointi 19 katika nafasi ya 18 ikiwa imecheza michezo 22, imeshinda michezo minne, imetoka sare michezo saba na imepoteza michezo 11.
Timu hiyo yenye maskani yake jijini Mwanza imesema ipo katika mchakato wa kutafuta mwalimu mwingine ili kurejea katika matokeo mazuri na kuinusuru na janga la kushuka daraja.
“Tunatoa shukran kwa kazi nzuri na ushirikiano waliotupa kipindi chote tulipokuwa nao na tunawatakia kila la kheri katika ukurasa wao mpya”, imeeleza taarifa iliyotolewa leo na Mbao FC.
Leo timu hiyo ina kibarua dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
