×

Nyosso: Bocco, Kagere Wana Hatari

Juma Nyosso

BEKI wa Kagera Sugar, Juma Nyosso ambaye anaaminika anakaba kwa akili na kutumia nguvu nyingi, amewasifu washambuliaji wa Simba, Meddie Kagere na John Bocco kutokana na kumpa wakati mgumu uwanjani.

 

Nyosso aliyasema hayo wakati juzi Jumanne Kagera ilipofungwa na Simba bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Katika mchezo huo, Kagere alifunga bao hilo kwa penalti dakika ya 61 iliyotokana na Bocco kufanyiwa faulo na kipa wa Kagera, Benedict Tinoko. Akizungumza na Spoti Xtra, Nyoso alisema, katika wachezaji waliompa wakati mgumu hadi sasa aliokutana nao msimu huu, ni Kagere na Bocco pekee.

“Bocco na Kagere ni washambuliaji wazuri ambao muda wote wanahitaji kufunga mabao, hivyo ilinibidi muda wote niwe nawakaba ili wasifunge japo nilifanikiwa kwa kiasi kadhaa, lakini bado ilikuwa ni ngumu kutokana na nguvu na kasi waliyonayo pindi wanapokuwa na mpira.

 

“Ilikuwa ni vigumu sana kuwakabili japo nilifanikiwa kwa kiasi chake, wapo tofauti na washambuliaji wengine ambao mara nyingi  huwa sipati shida sana ya kuwakaba,” alisema beki huyo.

 

Leave a Comment