TAARIFA zinadai kuwa Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limewajeruhi baadhi ya waandishi waliokuwa wakitelekeza wajibu wao wakati wa Kumkamata Mbunge wa Hai Freeman Mbowe (Chadema) aliyekuwa na mkutano wa hadhara kwenye eneo la Nkoromu.
Waandishi waliojeruhiwa ni Elia Peter wa Global TV Online na Janeth Joseph wa Mwananchi Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza na Global TV Online, Elia amesema mkutano huo umeisha kwa vurugu baada ya jeshi la Polisi kumchukua Mbowe kwa nguvu Jambo lililopelekea baadhi yao kupigwa hadi kufikishwa hospitali ya Wilaya ya Hai kwa Matibabu wakati wakitekeleza wajibu wao.
“Mwenzangu Janneth yupo hospitalini na kilichotokea ni kwamba Polisi waliokuja kumkamata Mbowe hawakutaka kupigwa picha ndipo walipomkamata na kumpiga na kitako cha bunduki na hata nlipotaka kumsaidia nao pia walinikamata na kunishambulia,” alisema Elia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamdun amesema Mbowe amekamatwa na polisi baada ya kutoa maneno ya uchochezi katika mkutano wake huo na kwamba yanaashiria uchochezi na kuamsha hisia za wananchi na chuki dhidi ya Serikali ya Tanzania na polisi.
“Mbowe amekamatwa na anashikiliwa na polisi baada ya kutuhumiwa kusema au kutoa maneno yanayoashiria uchochezi, kuamsha hisia na chuki dhidi ya Serikali na polisi. Anahojiwa lakini baada ya mahojiano atapewa haki ya dhamana,” amesema kamanda Hamdun.
Katika mkutano huo, Mbowe amesema hawezi kupongeza utendaji kazi wa Serikali mpaka atakapokuwa na uhakika Serikali inatenda haki kwa watu wote. Alikamatwa muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wa hadhara saa 11:58 jioni.
