×

Yanga: Simba Chukueni Tu Kombe, Kipigo Kinawahusu

SIMBA chukueni tu kombe, lakini kipigo kinawahusu, hii ni kauli ya Yanga ambayo wameitoa kuelekea mechi ya watani wa jadi, Machi 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Msimamo unaonyesha kuwa, Yanga ambao ni wenyeji hadi sasa wamepitwa na Simba pointi 21 lakini wana viporo viwili. Mechi ya mwisho baina ya timu hizo iliisha kwa sare ya mabao 2-2.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, kiongozi mmoja wa benchi la ufundi la Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina lake, alisema kuna mkakati kabambe ambao umepangwa ili kuhakikisha timu yao haipotezi mchezo huo.

 

Chanzo hicho kilisema kuwa, licha ya kutambua kuwa Simba wako kwenye nafasi nzuri ya kuwa machampioni lakini wamejipanga kutunza heshima yao kwa kuhakikisha wanawapiga Machi 8, pale Taifa ili kupunguza machungu.

“Simba waache tu wachukue ubingwa lakini Machi 8 tumeandaa mikakati lazima tuwafunge maana siku zote inajulikana Simba na Yanga zikitwaa ubingwa bila ya kuwafunga wapinzani wao ubingwa haunogi, hivyo lazima tuwafunge.

 

“Kocha Luc Eymael amewataka wachezaji wajitambue kwa kuhakikisha wanapata nafasi ya kuzungumza wenyewe kwa wenyewe uwanjani na kukosoana ili waweze kwenda sawa, wawe kama ndugu na kusitokee mtu akatofautiana na mwingine kwani ikitokea kutoelewana baina yao timu haitafanya vizuri.

 

“Kocha amewataka wachezaji kuhakikisha wanashinda michezo yote iliyobakia ili kuhakikisha wanaweka heshima ndani ya timu na ligi hata kama watakosa ubingwa,” alisema kiongozi huyo.

STORI: KHADIJA MNGWAI, Dar es Salaam

Leave a Comment