DAVID Molinga mshambuliaji wa Yanga jana aliwanyanyua mashabiki wa timu yake na kuwafanya wasitoke kizembe wakati ikishinda kwa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa.
Bao la kwanza la Yanga lilifungwa dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti na Molinga ambaye aliipiga kwa ufundi na kufunga bao lake la nane msimu huu.
Yanga ilifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chake jana ambapo sura mpya ziliibukia Taifa kwenye mchezo huo ambao ni pamoja Patrick Sibomana, Mrisho Ngasa, Farouk Shikalo na Papy Tshishimbi ambao wote waliukosa mchezo uliopita dhidi ya Alliance FC.
Majembe ya kazi kama Metacha Mnata, Erick Kambamba, Bernard Morrison yalianzia benchi kuusoma mchezo huo wakiivutia kasi Machi 8.
Patrick Sibomana katika dakika ya 81 aliifungia bao la pili kwa krosi iliyopigwa na Tariq Seif.
Huu ni ushindi wa pili mfululizo Yanga wanaupata, walianza mbele ya Alliance FC jana ilikuwa zamu ya Mbao FC zote kutoka kanda ya ziwa na zimefungwa mabao 2-0.
Molinga alionekana mwenye furaha baada ya kufunga bao lake la nane ndani ya ligi huku akiwaambia mashabiki kwa ishara kwamba watulie kuna jambo kubwa litafanyika kwenye uwanja huo.
Machi 8, Yanga itawakaribisha Simba Uwanja wa Taifa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao utakuwa ni mzunguko wa pili na inaonekana kwamba kwa ushindi walioupata jana itaongeza morali na nguvu kwa wachezaji wao.
Ushindi huu umewafanya Yanga wafikishe pointi 47 baada ya kucheza michezo 24 wakisogea hadi kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.
Chanzo: Omary Mdose, Dar es Salaam

