×

Anayehubiri kwa nyoka kuibuka bongo!

WAKATI maombezi kwa kutumia mafuta ya upako yakitikisa Bongo, mchungaji anayeombea kwa kutumia nyoka, mbioni kuja nchini kusimika huduma yake, chanzo kimeliambia Risasi Mchanganyiko.

Chanzo hicho kimesema kuwa mchungaji Lesego Daniel wa kituo cha maombezi cha Rabboni nchini Afrika Kusini, anayetikisa kwa staili ya kuombea watu kwa nyoka aliyehai, anatarajiwa kufika Bongo mwishoni mwa mwezi ujao. “Nimekuwa katika harakati za kutafuta usajili wa huduma yake kama alivyoniomba, nimefikia mahali pazuri.

“Maana lengo lake si tu kuleta huduma hiyo ya kiroho yenye nguvu za ajabu za Kimungu, lakini pia amepanga kufungua tawi hapa,” alisema Charles Masanja ambaye alijitambulisha kuwa ni mtumishi wa Mungu anayeishi Tegeta jijini Dar es Salaam.

Aidha, Masanja aliongeza kuwa amefahamiana na mtumishi huyo wa Mungu aishiye Afrika Kusini kwa njia ya mitandao na kwamba kwa hapa nchini, yeye atakuwa msaidizi wake.

Uchunguzi uliofanywa na Risasi, umebaini kuwa mchungaji Lesego ndiye aliyekuwa akitoa huduma ya maombezi nchini Afrika Kusini kwa kuwalisha majani mabichi na kuwanywesha mafuta ya petroli waumini wake na kwamba, kinachotokea hivi sasa kuhusu kuhubiri kwa kutumia nyoka, ni kama mchungaji huyo amekuja na gia nyingine ya kuombea watu.

Hata hivyo, pamoja na mchungaji Lesego kutoa huduma zake kwa kutumia staili za kushangaza, jambo la kustaajabisha zaidi ni kwamba watu wengi wakiwemo wasomi, wamekuwa wakimiminika kanisani kwake kufuata huduma za aina hiyo.

Mwandishi wetu alipomuuliza Charles kuhusu huduma hiyo ya kuhubiri kwa kutumia nyoka imewahi kufanywa wapi katika historia ya kanisa alisema:

“Anhaa unataka kujua nyoka alitumika wapi katika kufanya miujiza? Kasome maandiko katika kitabu cha Kutoka 7: 9-13,” alisema kwa kujiamini.

Maandiko katika kitabu hicho yanasomeka hivi: “Ikiwa Farao atanena nanyi, na kusema, ‘Jifanyieni muujiza,’ basi utamwambia Haruni, ‘Chukua fimbo yako, uitupe chini mbele ya Farao.’ Itakuwa nyoka mkubwa.”

“Kwa hiyo Musa na Haruni, wakaingia ndani kwa Farao na kufanya sawasawa na vile ambavyo Yehova alikuwa ameamuru. Basi Haruni akaitupa chini fimbo yake mbele ya Farao na watumishi wake, nayo ikawa nyoka mkubwa. Hata hivyo, Farao pia aliwaita watu wenye hekima na walozi; na makuhani wa Misri wenye kufanya uchawi, nao pia wakafanya jambo hilo hilo kwa ufundi wao wa uchawi. Kwa hiyo, kila mmoja wao akatupa chini fimbo yake, nazo zikawa nyoka wakubwa; lakini fimbo ya Haruni ikameza fimbo zao.”

Siku za hivi karibuni wameibuka wachungaji mbalimbali, ambao wamekuwa wakitumia staili tofautitofauti kuombea watu na kujipatia wafuasi wengi, jambo ambalo kwa upande mwingine limekuwa likipingwa na baadhi ya wachungaji kwa kudai kuwa miujiza inayofanywa na watumishi wa aina hiyo ni ya kishetani.

Askofu wa Kanisa la Full Gosper Bible Fellowship ‘FBGF’ jijini Dar es Salaam, Zachary Kakobe hivi karibuni aliwaonya waumini wake kuacha kukimbilia miujiza ya shetani inayofanywa na wachungaji wasiotumia jina la Yesu kuombea watu, kwani itawapeleka motoni.

STORI: Mwandishi Wetu, Risasi

Leave a Comment