×

Nchimbi: Kocha Akinipanga, Siwaachi Simba SC

MSHAMBULIAJI mwenye jina kubwa hivi sasa Yanga, Ditram Nchimbi amesema kama kocha wake Mbelgiji Luc Eymael atampanga katika kikosi cha kwanza, basi hatawaacha watani wao, Simba.

 

Timu hizo zinatarajiwa kuvaana keshokutwa Jumapili kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara unaosubiriwa kwa hamu kubwa utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 

Nchimbi amekuwa kwenye kiwango bora siku za hivi karibuni ambapo kwenye mchezo dhidi ya Alliance FC alifunga mabao yote mawili ya Yanga waliposhinda mabao 2-0.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Nchimbi alisema kuwa mchezo dhidi ya Simba ni mgumu na usiotabirika kutokana na upinzani na presha inayokuwepo kwa mashabiki.

 

Nchimbi alisema kwao wachezaji hawana hofu kutokana na kuwakutanisha wachezaji wanaojuana, hivyo kwake atahakikisha anautumia mchezo kujitangaza akiamini mawakala wengi watakuwepo uwanjani kuufuatilia.

 

“Lipo wazi mchezo wa watani wa jadi ni wa heshima, hivyo kama nitapewa nafasi ya kucheza siku hiyo, basi sitawaacha hao Simba kutokana na umuhimu mkubwa ninaouchukulia mchezo huu.

 

“Hakuna ubishi mchezo dhidi ya Simba ni mgumu usiotabirika kutokana na upinzani uliopo kati ya timu hizo mbili zinapokutana, presha kubwa inakuwepo kwa mashabiki pekee lakini siyo kwa wachezaji.

 

“Uzuri zaidi mchezo huu unaweza kukupaisha au kukushusha chini kama hutafanya vizuri. Mimi binafsi nimejipanga kuhakikisha nafanya vizuri kama kocha atanipa nafasi,” alisema Nchimbi aliyefunga mabao matano hadi hivi sasa.

Stori: Mwandishi Wetu

Leave a Comment